
Kuna tabia fulani mbaya unaweza kuziona kwa mtu anayesema ameokoka, ukashindwa kuelewa sana kutokana na matendo yake yalivyo. Maana unaweza ukawa unamwona ni mtu wa kanisani sana ila haachi maseng’enyo, haachi kugombana na watu.
Kama ni mtaani utamkuta ni mama anayeongoza kwa kugombana na wamama wenzake, sababu haswa inayomfanya mama au dada huyu agombane na wenzake mtaani ni tabia yake ya maneno ya uchonganishi.
Lakini mama huyu huyu au dada huyu huyu akiwa kanisani ni mtu anayeonekana ana busara sana, ni mtu anayeonekana ametulia sana, ni mtu anayeonekana hapendi mambo mabaya.
Pamoja na kuvaa ngozi ya upole akiwa maeneo ya kanisani, mtaani kwake au ofisini kwake anajulikana kwa majina mabaya yasiyo na sifa njema kabisa. Barua yake inasomeka vibaya sana kwa watu wasiomjua Yesu na wanaomjua Kristo.
Watu kama hawa ni watu wenye tabia ya mwilini, watu ambao bado wana mambo ya Dunia, watu ambao wanatamka kwa vinywa vyao wameokoka lakini bado ndani yao ni wachanga sana kiroho.
Watu kama hawa wanahitaji mafundisho sahihi ya Neno la Mungu, mafundisho ambayo yatawasaidia kuwaondoa kwenye hatua ya uchanga wa kiroho, na kuwapeleka kwenye hatua ya ukomavu wa kiroho.
Hebu waone watu hawa wa mwilini kupitia andiko hili hapa, uone tabia zao zilivyo, huenda ukafikiri ninayokueleza hapa hayapo. Amini yapo, na watu wa namna hii tunao kwenye mazingira yetu.
Rejea: Kwa maana hata sasa ninyi ni watu wa tabia ya mwilini. Maana, ikiwa kwenu kuna husuda na fitina, je! Si watu wa tabia ya mwilini ninyi; tena mnaenenda kwa jinsi ya kibinadamu? 1 KOR. 3:3 SUV.
Mtu yeyote unayemwona ana tabia ambazo haziendani na sifa za mkristo, ujue huyo ni mtu wa tabia ya mwilini, mtu anayeenenda kwa jinsi ya kibinadamu.
Mtu ambaye anahitaji msaada wa kiroho, mtu ambaye anahitaji mafundisho ya Neno la Mungu ya kutosha, mtu ambaye anapaswa kujibidiisha yeye mwenyewe kusoma Neno la Mungu.
Bila kupata hayo, ataendelea kuwa hivyo huku akijua anachofanya yupo sahihi, maana zipo tabia haziondolewi kwa maombi, bali huondolewa pale mtu anapopata mafundisho sahihi ya Neno la Mungu.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com