Unapojitenga na mambo mabaya na kuamua kuokoka sawasawa, usifikiri utakuwa umejiepusha na kila kitu, yapo mambo mabaya utayapata kwa kusikia ama kwa kuona kwa macho yako.

Kuwa ndani ya Yesu Kristo unakuwa salama ila sio kwamba hutotupiwa maneno yasiyofaa, sio kana kwamba hutosingiziwa mambo mabaya, sio kana kwamba hutotukanwa, na sio kana kwamba hutosingiziwa mambo mabaya.

Watu wengine wakishaona wanaandamwa na maneno mabaya huwa wanashindwa kuhimili hayo na kuanza kujibu mashambulizi kwa njia ambayo haimpendezi Mungu. Badala ya kuonekana kama watu waliokoka wanageuka na kuonekana watu wasiomjua/wasiomwamini Yesu.

Hakuna mtu anayependa kutukanwa, wala hakuna mtu anayependa kuudhiwa, wala hakuna mtu anayependa kusingiziwa jambo ambalo hakulifanya.

Pamoja na kutopenda hayo yote, pamoja na umeokoka sawasawa, hutoacha “KUTUKANWA” na watu wasiojua Neno la Mungu, utasema kwanini utukanwe na wakati hakuna ulichokosea? Hiyo ipo ndugu yangu huna la kukwepa, cha msingi ni kuwa na maarifa sahihi ya Neno la Mungu, ili ujue namna ya kufanya pale unapokutwa na hili.

Pamoja na kuokoka kwako vizuri, kaa ukijua hutoacha “KUUDHIWA” iwe kwenye kazi yako utaudhiwa na wafanyakazi wenzako au viongozi wako au viongozi wenzako, iwe kwenye ndoa yako utaudhiwa na mume/mke wako, iwe kwenye kwaya utaudhiwa tu, iwe huduma yako yoyote ile ujue utaudhiwa.

Pamoja na Mungu kujitukuza kupitia huduma yako unayoifanya ya kumtumikia Mungu, usifikiri utaepukana na hili la “KUSINGIZIWA”. Usishangae unaambiwa unatembea na mke/mume wa mtu, usishangae unaambiwa wewe ni mchawi, usishangae unaambiwa unatumia nguvu za giza kuponya watu wenye shida mbalimbali.

Usishangae unaambiwa utajiri ulionao ni kwa sababu uliua mtoto wako au mzazi wako au ndugu yako, kumbe mtoto wako au mzazi wako au ndugu yako alikufa tu, kwa sababu siku yake ilifika. Sio kana kwamba hicho kifo ulisababisha wewe ili upate mali nyingi, ni kifo tu kama vifo vingine vinavyoweza kumtokea mtu yeyote.

Sasa unapokutana na hali hizi tatu, yaani kutukanwa, kuudhiwa, na kusingiziwa, huwa unafanyaje? Nakuuliza hivi kwa sababu ni mambo ambayo utakuwa umekutana nayo, na kama bado vizuri kufahamu haya vizuri. Na siku hizi kuna mitandao ya kijamii, unaweza kutukanwa kwenye mitandao kwelikweli, na unaweza kusingiziwa jambo likaonekana mbele za watu ni la kweli, kumbe ni la uongo.

Hebu tuone maandiko matakatifu yanasemaje kuhusu hili, vizuri kujenga tabia ya kusoma Neno la Mungu kila siku, bila kuwa na maarifa sahihi ya Neno la Mungu huwezi kuhimili hayo niliyokutajia pindi yatakapokukuta. Ama unaweza kupambana isivyo kustahili kama mtu aliyeokoka sawasawa.

Rejea: Kisha twataabika tukifanya kazi kwa mikono yetu wenyewe. Tukitukanwa twabariki, tukiudhiwa twastahimili; tukisingiziwa twasihi; tumefanywa kama takataka za dunia, na tama ya vitu vyote hata sasa. 1 KOR. 4:12‭-‬13 SUV.

Unaona hilo andiko linavyosema? nataka utazame yale maneno yanavyosema hivi; Tukitukanwa twabariki, tukiudhiwa twastahimili; tukisingiziwa twasihi. Je! Mara ngapi umetukanwa ukabariki? Mara ngapi umeudhiwa ukastahimili? Mara ngapi umesingiziwa ukawasitahi au ukawajibu kwa maneno ya hekima au ukakaa kimya baada ya kuona huna haja kuwajibu wale wanaokusingizia vitu vya hovyo.

Hapa tunajifunza maandiko matakatifu vile yanavyosema, kama unafanya huduma au kama umeokoka sawasawa utakuwa umekutana na kitu kimoja wapo kati ya hivi, kutukanwa, kuudhiwa, kusingiziwa, lazima utakuwa umekutana na hivi vitu.

Inawezekana kabisa umekutana na vyote vitatu, au inawezekana umekutana na viwili kati ya hivyo vitatu, au inawezekana umekutana na kimoja kati ya hivyo vitatu. Sina uhakika kama upo hapa duniani na unamtumikia Mungu au umempa Yesu Kristo maisha yako, alafu uwe hujawahi kukutana na hivi vitu, ni kitu kisichowezekana.

Wakati mwingine unaweza ukawa umeshindwa ufanyaje pale ulipokutana na haya, kupitia maandiko haya naamini utakuwa umejifunza namna ya kufanya pale utakapokutana na hali moja wapo kati ya hizi tulizojifunza leo.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com