Kuna vitu vinatendeka kwenye vikundi vyetu mbalimbali, viwe vya kwaya, viwe vikundi vya vijana, viwe vya maombi, au vinaweza vikawa vikundi zaidi vya hivi nilivyokutajia hapa.

Kati ya vikundi hivi anaweza akawepo mtu mwenye tabia mbaya, tabia ambayo inaleta picha mbaya ya kundi hilo, tabia ambayo inaambukiza na watu wengine ndani ya kundi, tabia ambayo haionyeshi kushtua watu wengine na wakati ni tabia mbaya.

Watu kama hawa wasipokemewa, wasipoonywa, wasipoambiwa wanachofanya hakitakiwi ndani ya kundi lenu, na asipoambiwa akiendelea kufanya anachofanya ataondolewa kwenye kundi hilo.

Uwe na uhakika mtu huyo ataendelea kufanya hicho kibaya anachofanya bila kuwa na hofu yeyote, anaweza kujiona anachokifanya kipo sahihi kabisa. Maana hakuna kiongozi anayemwambia kitu chochote, wala hakuna mtu yeyote anayeinuka kumwambia unachofanya sio kitu kizuri.

Ukikuta mtu wa namna hiyo yupo ndani ya kundi, halafu hakuna mtu anayenyanyua mdomo wake kumwambia hicho unachofanya sio kizuri. Watu hao mara nyingi hufikiri wakimwambia au wakimwonya au wakimkemea, wanaona watampoteza kwenye kundi lao.

Wanaona ni bora kukaa kimya huku mtu akiendelea kufanya mambo yasiyofaa, mambo ambayo ni chukizo mbele za Mungu, mambo ambayo yanaambukiza hata wale washirika wengine wasiokomaa kiroho.

Maana wapo watu wakishaona mambo mabaya yanayofanywa hayakemewi na viongozi wa kundi, mara nyingi huona ni sahihi kufanya hivyo. Kumbe sio sahihi hicho kinachofanywa, bali ni dhambi mbele za Mungu.

Tena watu wengine huwa wanaona ni vibaya kumwondoa mtu anayefanya mambo mabaya, mambo ambayo ni chukizo mbele za Mungu, mambo ambayo ni mbegu mbaya kwa kundi. Pamoja na kuonywa sana mtu huyo kuhusu tabia yake mbaya akawa hasikii, watu wengine huona kuondolewa kwenye kundi huwa sio sawa.

Huwa wanaona ni heri akaachwa akaendelea kuwepo kwenye kundi kuliko kuondolewa, wao hufikiri wanapomwacha aendelee kuwepo kwenye kundi ni sahihi. Maana hata Yesu Kristo alikaa na wanyang’anyi, na wao wanafikiri kuendelea kukaa na huyo mtu ni sahihi.

Ndio maana ni muhimu sana kuwa na Neno la Mungu la kutosha moyoni mwako, bila kuwa na Neno la Mungu la kutosha moyoni unaweza kushikilia andiko moja isivyo sahihi. Alafu ukaendelea kuambatana na rafiki asiye sahihi, rafiki ambaye anafika mahali anakuambukiza tabia yake mbaya, hiyo sio sawa.

Hebu tuone maandiko matakatifu yanasemaje kuhusu hili jambo ninalokueleza hapa, tuone vile ilivyo na athari kukaa kimya huku unamwona mtu anafanya mambo mabaya. Tena kuendelea kumfurahia bila kuonyesha hali yeyote ya kusikitika kwa matendo yake mabaya.

Rejea: Yakini habari imeenea ya kuwa kwenu kuna zinaa, na zinaa ya namna isiyokuwako hata katika Mataifa, kwamba mtu awe na mke wa babaye. Nanyi mwajivuna, wala hamkusikitika, ili kwamba aondolewe miongoni mwenu huyo aliyetenda jambo hilo. 1 KOR. 5:1‭-‬2 SUV.

Unaona hilo andiko linavyosema, wapo watu wanaweza kujivuna kwa zile tabia mbaya za mtu, bila kuonyesha masikitiko yeyote, ili huyo mtu aondolewe kwenye kundi kama atakuwa ameshindwa kusikia alichoambiwa/alichoonywa.

Badala yake tumewaacha wale watu kwenye makundi, baada ya muda makundi yetu yamesambaratika au baada ya muda makundi yetu yameonekana ni makundi ya kihuni. Makundi ambayo hayafai kabisa mtu mwenye safari ya kwenda mbinguni kukaa mahali pale.

Vizuri kulifahamu hili, kama ni kiongozi wa kundi au kama ni mtu ambaye upo katikati ya kundi, alafu ukawa unaona tabia mbaya za mtu fulani ndani ya kikundi chenu. Hupaswi kukaa kimya hata kidogo, kama una uwezo wa kumwonya huyo mtu ni vizuri kufanya hivyo, umejiona huwezi ni afadhali kulifikisha kwa uongozi.

Hupaswi kufumbia macho mambo mabaya, wala hupaswi kuchekea mtu mwenye tabia mbaya, tena unapaswa kukaa naye mbali, wala hupaswi kushirikiana na mtu huyo kila kitu.

Naomba unielewe hapa, unapaswa kuwa makini sana, ukiwa na mazoea ya karibu sana na watu au mtu mwenye tabia fulani mbaya, ukawa unashirikiana naye baadhi ya maeneo kama rafiki yako wa karibu. Ipo siku na wewe utakuwa ni mtu ambaye unafanya kile kile kibaya.

Rejea: Naliwaandikia katika waraka wangu, kwamba msichangamane na wazinzi. Sisemi msichangamane kabisa na wazinzi wa dunia hii, au na wenye kutamani, au na wanyang’anyi, au na wenye kuabudu sanamu; maana hapo ingewalazimu kutoka katika dunia. Lakini, mambo yalivyo, naliwaandikia kwamba msichangamane na mtu aitwaye ndugu, akiwa ni mzinzi au mwenye kutamani au mwenye kuabudu sanamu au mtukanaji au mlevi au mnyang’anyi; mtu wa namna hii msikubali hata kula naye. 1 KOR. 5:9‭-‬11 SUV.

Hayo maandiko matakatifu nimekupa, yasome kwa umakini, usifikiri tu kila mtu ni wa kuchangamana naye, kuna watu unapaswa kuwa nao makini sana. Tupo duniani na tunaishi na watu wenye tabia mbalimbali mbaya, hiyo sio sababu sana ya kujitetea, bali unapaswa kujua ni mambo gani ya kushirikiana nao.

Nimalize kwa kusema kwamba, kusoma Neno la Mungu ni jambo la muhimu sana kwa mkristo mwenye nia ya kuishi maisha ya kumpendeza Mungu wake. Bila kuwa Neno la Mungu la kutosha moyoni mwako, uwe na uhakika utamtenda Mungu dhambi.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com