
Itakuwa ngumu sana kama tutakuwa tunasema Yesu Kristo ni Bwana na mwokozi wa maisha yetu, lakini ndani ya mioyo yetu tunakuwa hatuna kabisa imani kama Yesu yupo na anaweza kutusaidia.
Kinachotufanya tumpendeze Mungu wetu, kinaweza kuonekana ni kidogo kwa kutamka kwa maneno ila ndicho kinapaswa kuzingatiwa sana, ili tuweze kumpendeza Mungu wetu.
Kumpendeza Mungu wetu ni kuishi maisha matakatifu hilo linafahamika kwa watu wengi, lakini pamoja na mtu anapaswa kuishi maisha matakatifu. Mtu huyo anapaswa kuwa na imani ya kwamba Mungu yupo.
Bila kuwa na imani kuwa Mungu yupo, haiwezekani kabisa kumpendeza Mungu wetu, tunajilinda na mabaya ya Dunia, kwa sababu tunayo imani ndani yetu kuwa Mungu hapendi dhambi, wala hapendi mtu mwenye mashaka naye.
Kama una imani ya kusitasita, huna imani kama Mungu yupo, huna imani kama Mungu anaweza kukusaidia jambo, huna imani kama Mungu anaweza kukuponya, huna imani kama Mungu anaweza kukutoa kwenye hatua moja kwenda nyingine.
Uwe una uhakika hutoweza kumpendeza Mungu katika maisha yako, mtu anayeweza kumpendeza Mungu ni yule ambaye anaamini Mungu yupo. Huyo ataishi maisha ya utakatifu, maisha ambayo ni ya kujichunga sana.
Tena mtu anapomwendea Mungu kwa maombi, lazima awe na imani na yule anayemwendea, tena anapaswa kuamini kuwa Mungu yupo. Sasa kuna watu wanaenda mbele za Mungu ila hawaamini kama yupo yule ambaye anaweza kuwasaidia shida zao.
Rejea: Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza; kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao. EBR. 11:6 SUV.
Ndugu ili uweze kumpendeza Mungu wako, lazima uwe na imani naye, tena unapoenda mbele zake kwa maombi, kabla hujaanza kuomba unapaswa kumwamini yule unayemwendea kumwomba yupo.
Usiende mbele za Mungu kuomba, alafu ukawa huna imani naye, imani yako mbele za Mungu ni ya muhimu sana. Ndani yako inapaswa kujengeka imani iliyo thabiti juu ya Mungu, hapo ndipo utaweza kumpendeza Mungu.
Utaona matendo makuu yakidhihirika kwa matendo ya mwili, kwa sababu ya imani yako mbele za Mungu, utaona majibu ya mahitaji yako uliyomwomba Mungu, kwa sababu ya imani yako mbele za Mungu. Imani yako mbele za Mungu inaweza kuvuta majibu ya maombi yako.
Ukiwa kama mtu uliyeokoka na mwenye safari ya kwenda mbinguni, hakikisha unakuwa na imani, pasipo imani huwezi kumpendeza Mungu. Upo tayari kufuata ushauri ulioambiwa na watu wasiomjua Yesu Kristo, na shida ushauri huo ulio kinyume na Neno la Mungu ukaufuata, kwa sababu ya kukosa imani mbele za Mungu.
Na ili imani yako ijengeke vizuri ndani yako, lazima uwe na Neno la Mungu la kutosha, kinachofanya imani yako ijengeke vizuri ndani yako ni kusikia mafundisho ya neno la Mungu au kusoma Neno la Mungu.
Rejea: Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo. Warumi 10:17.
Imani iliyo imara haiji hivi hivi, lazima uitafute kwa gharama, lazima uwe na bidii kwenye kusoma Neno la Mungu kila siku, lazima uwe na bidii ya
kuhudhuria mafundisho mbalimbali ya Neno la Mungu.
Ukifanya hivyo utaanza kuona imani yako ikianza kujengeka ndani yako, sio unatumia muda mwingi kwenye vitu visivyohusiana na Neno na Mungu, wala na mafundisho ya Neno la Mungu. Alafu utegemee utakuwa na imani safi inayoweza kumpendeza Mungu wako, ni kitu kisichowezekana.
Hakikisha msingi wa imani yako unajengwa kwenye Neno la Mungu, hili ni la muhimu sana kuzingatia ukiwa kama mkristo mwenye safari ya kwenda mbinguni. Usijenge msingi wa imani yako nje na Neno la Mungu, utaingia hasara kubwa.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com