Miongoni mwa watu ambao wamekuwa wakikutana na maneno mazito na ya hovyo, watu ambao wamekuwa wakitukanwa matusi mabaya, watu ambao wamekuwa wakionekana wanafuatilia sana maisha ya watu.

Watu ambao wameonekana hawana kazi za maana za kufanya, wakati mwingine wamekosa idadi kubwa ya marafiki, hasa wale watu ambao njia zao hazipo vizuri mbele za Mungu. Huwa wanaowaona wale wanaojaribu kuwaonya juu ya tabia zao mbaya wanafuatilia maisha yao.

Watu waliotoa maisha yao kwa Bwana, watu ambao wanakemea dhambi, watu ambao wanaonya wale wanaotenda mabaya, watu ambao wanafundisha kweli ya Mungu. Watu ambao Hawakwepeshi neno pale wanapoona mambo hayaendi kama Neno linavyosema waende.

Watu hao hupata maneno magumu sana kwenye maisha yao ya huduma, watu ambao walitakiwa kuwa watu wanaopendwa sana. Lakini shetani anaingiza chuki ndani ya mioyo ya wale ambao anawatumikisha kwenye kazi zake ovu, wanakuwa wanawaona wale wanaowaambia ukweli ni watu wabaya.

Ubaya wa wale wanaowaambia ukweli, unakuwa ni ukweli wao, wanakuwa wanawaona wanafuatilia maisha yao. Lakini ukija kwenye ukweli wanakuwa wanawasaidia, ili kuponya nafsi zao mbele za Mungu.

Wasilolijua hawa watu wanaosema waache kufuatiliwa maisha yao, hadi wanafika mahali ambapo wanasema “ACHANA NA MIMI FUATA YAKO” hawajui kupitia wao kuna watu watadaiwa damu zao mbele za Mungu.

Wanachojua wao ni waache kufuatiliwa maisha yao ila hawajui kupitia wao kuna watu wana deni mbele za Mungu, wataulizwa kwanini hawakuwaambia waache njia zao mbaya, na yupo ataulizwa kwanini hukumwambia ndugu yako aache tabia yake mbaya.

Kuacha au kutokuacha kwa mtu mwenye tabia mbaya ni suala lingine ila la msingi ulimwambia? Na kama hukumwambia utadaiwa damu yake mikononi mwako. Sasa mtu asiyejua anaona mtu anayemwambia ukweli anakuwa amekosa kazi za kufanya, anaonekana hayupo bize ndio maana ana muda wa kufuatilia maisha ya watu.

Inawezekana ndugu msomaji wangu umekuwa miongoni mwa wa watu wanaoona wanafutiliwa maisha yao, umefika mahali unawatupia maneno magumu wale wanaokuonya kuhusu tabia yako mbaya. Kuanzia sasa fahamu hiyo ni kazi ya watu wanaopenda kwenda mbinguni, wakikaa kimya bila kukuambia ukweli elewa watadaiwa.

Rejea: Nimwambiapo mtu mbaya, Hakika utakufa; wewe usimpe maonyo, wala husemi na huyo mtu mbaya ili kumwonya, kusudi aache njia yake mbaya na kujiokoa roho yake; mtu yule mbaya atakufa katika uovu wake; lakini damu yake nitaitaka mkononi mwako. Ezekieli 3:18.

Nani anataka kudaiwa damu yako mikononi mwake, nani anataka kudaiwa damu ya ndugu yake au rafiki yake mikononi mwake, hakuna mkristo yeyote mwenye safari ya kwenda mbinguni anayetaka kukutana na hili jambo.

Mtu yeyote aliye na Neno la Mungu la kutosha moyoni mwake, na mtu yeyote anayejua madhara ya kunyamazia uovu, hawezi kukuangalia ukifanya upuuzi wako. Lazima atakuambia, lazima atakufuatilia, mtu anataka asifuatiliwe alafu anasema ameokoka, kwanini asifuatiliwe na wakati ametangaza kuokoka?

Yeye ni nani asifuatiliwe, maana sisi tuliokoka ni barua inayosomwa na kila mtu, awe ameokoka au awe hajaokoka, utafuatiliwa nyendo zako. Maana waliokoka wanajulikana wanapaswa waweje, na wasiokoka nao wanajulikana wanapaswa waweje.

Umeokoka na unaonekana unaenda ndivyo sivyo lazima watu waongee, lazima watu wakujie na kukuonya kuhusu kile unafanya, lazima uelekezwe kuhusu hicho unachofanya sio sahihi.

Haijalishi ulikuwa umeokoka sawasawa siku za nyuma, kama umeiacha njia sahihi, unapoambiwa ukweli usijione unaelewa sana ukristo ukawa hutaki kuambiwa kitu. Kama umeiacha njia sahihi, wewe unahitaji msaada wa Mungu, na huna mamlaka ya kuwaambia watu wafuate yao.

Rejea: Tena mtu mwenye haki aiachapo haki yake, na kutenda uovu, nami nikiweka kikwazo mbele yake, atakufa; kwa sababu hukumwonya, atakufa katika uovu wake, wala matendo yake ya haki aliyoyatenda hayatakumbukwa; lakini damu yake nitaitaka mkononi mwako. Ezekieli 3:20.

Hakuna mtumishi anayetaka ufe kwenye uovu wako, alafu mtumishi huyo akadaiwe damu yako mikononi mwake. Kwa hiyo uonapo mtumishi au mshirika yeyote unayemwona wewe ni wa kawaida, anakuambia acha hilo baya, ujue yupo kwenye nafasi yake sahihi kabisa.

Usione watu wamekosa kazi za kufanya, hadi unafika hatua unawaambia “ACHANA NA MIMI FUATA YAKO” wakati kukufuata wewe na kukuambia ni moja ya majukumu yao. Isipokuwa wewe hujui kuwa wapo kwenye majukumu yao, utawaona wanajipendekeza au wamekosa cha kufanya.

Na kama ulikuwa unaogopa kuonekana mbaya, huwa unawaacha watu wafanye mambo yao mabaya huku ukiwaangalia tu kwa macho yako. Wakati mwingine unasema watajua wenyewe, uwe na uhakika kunyamaza kwako kutakuumiza siku ya mwisho.

Ndio maana unapaswa kujua maandiko matakatifu yanasemaje, kuwa tu mkristo bila kuwa na Neno la Mungu moyoni mwako. Unaweza ukawa unaishi maisha ya kumkosea Mungu wako huku wewe unakuwa unajua upo vizuri.

Soma Biblia yako kila siku, lijaze Neno la Mungu moyoni mwako vya kutosha, kama hili la kusoma Neno la Mungu ni changamoto kwako, karibu kwenye kundi letu la wasap la kusoma Neno la Mungu kila siku. Tuma ujumbe wako kwa wasap namba +255759808081 utaunganishwa.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com