Kinachotuangusha wengi ni pale tunapofika hatua tunajiona tayari tumeshajua kila kitu hatuhitaji tena kujifunza kwa wengine, ama hatuhitaji kuendelea kupata maarifa kutoka kwenye vitabu mbalimbali.

Mtu kufikiri tu ameshajua mambo mengi hahitaji tena kujifunza chochote kile kwa wengine, tayari mtu huyo ameshatangaza kuanguka kwake. Maana anachofikiri sio sahihi kabisa, maana hakuna mtu anayefikia kiwango cha kujua kila kitu.

Haijalishi unajiona moyoni mwako unajua sana Neno la Mungu, unachojua ni kijisehemu kidogo sana, sehemu nyingine yote iliyobaki huijui kabisa. Hata kama utakataa hili ninalokuambia, fahamu kwamba bado hujui kwa kiwango kikubwa.

Haijalishi umesoma sana vitabu vingi, unayopaswa kuendelea kuyajua ni mengi sana kuliko uliyonayo ndani ya fahamu zako. Unavyofikiri umetosheka na maarifa uliyonayo, huko ni kujidanganya kabisa, unachokijua ni kidogo sana.

Ndio maana unapaswa kusoma Neno la Mungu kila siku, bila kujalisha umeshasoma Biblia yote kuanzia kitabu cha mwanzo hadi ufunuo. Unapaswa kuendelea kulisoma Neno la Mungu na kulitafakari kila siku, yaani kila siku.

Changamoto inakuja pale mtu anapopata nafasi ya kumaliza kusoma Biblia yote, na labda awe amepata nafasi ya kusoma chuo cha Biblia. Mtu huyo anakuwa anaona anajua kila kitu, jambo ambalo sio kweli kabisa na anakuwa anajipoteza mwenyewe.

Ukweli ni kwamba hakuna mtu aliyefikia kiwango cha kutokutaka kujifunza tena, yeyote anayefikiri ameshajua kila jambo/kitu na hahitaji kujifunza kwa wengine au hahitaji kujifunza kutoka vitabuni mtu huyo amepotea njia.

Unaweza ukamwona mtu ana kiwango kikubwa sana cha ufahamu wa maarifa sahihi, pamoja na kuonekana hivyo mtu huyo bado hajajua kila kitu hadi kufikia hatua ya kutojifunza, anahitaji kuendelea kujifunza zaidi.

Ndivyo hata maandiko matakatifu yanatuambia hivyo, usifikiri ni maneno yangu, hichi ninachokueleza hapa kipo kimaandiko. Na nataka ulione hili jambo kwa mtazamo chanya ili uweze kusaidika na hili somo.

Rejea: Mtu akidhani ya kuwa anajua neno, hajui neno lo lote bado, kama impasavyo kujua. 1 KOR. 8:2 SUV.

Haleluya, unaona hilo andiko, kumbe hata yule anayejua, bado hajajua kama impasavyo kujua. Pamoja na kujua ameshajua, kupitia andiko hili mtu huyo anaonekana hajajua kama impasavyo kujua.

Kwa maana nyingine tunaweza kusema kwamba, kama mtu anajua kitu, atakuwa anajua robo yake au theluthi yake, maana yake anapaswa kuendelea kujifunza hadi atapofikia kitu kizima. Ambapo na hilo nalo linaweza likawa jambo gumu kwake/kwetu.

Acha kabisa kiburi cha maarifa machache uliyonayo na kujiona huna haja ya kujifunza kwa watu wengine, huko ni kujinyima nafasi ya kuendelea kufahamu mambo mengi zaidi.

Kujifunza nakufananisha na kula chakula, mtoto anazaliwa anaanza kunyonya maziwa ya mama yake, anatoka kunyonya anaanza kupewa uji au maziwa ya ng’ombe. Baadaye anakomaa na kuanza kula kila chakula, lakini hakuna siku alifika akasema ametosheka hahitaji tena kula chakula chochote.

Mtu anafunga siku kadhaa au masaa kadhaa ila haijawahi kutokea mtu akasema anaacha kabisa kula chakula chochote, ukiona anasema anaacha kabisa kula ujue huyo mtu ameshajitangazia kifo. Bila kupata msaada wowote wa kimawazo anaenda kupoteza uhai wake.

Mwisho, niseme kwamba kujifunza hakuna ukomo, na unapaswa kufahamu kwamba kile unachofikiri unakijua, unakijua kwa kiasi kidogo sana. Lakini kadri utakavyozidi kujifunza ndivyo utakavyozidi kujua zaidi.

Kama bado hujajiunga na kundi la wasap la kusoma Neno la Mungu kila siku kwa mtiririko mzuri, chukua hatua ya kujiunga sasa. Tuma ujumbe wako wasap namba +255759808081 utaunganishwa baada ya kupewa kanuni za kundi.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com