Nimewahi kusikia watu baadhi wakisema sina haja na mwanaume, na wengine sina haja na mwanamke, hii ni baada ya kuumizwa na mahusiano yao. Wakaona hawana haja kabisa na mwanamke/mwanaume ila katika uhalisia kila mmoja anamhitaji mwenzake.

Mfumo wa maisha yetu jinsi ulivyotengenezwa na Mungu wetu, kila mmoja anamhitaji mwenzake, hakuna mtu ambaye anasema yeye anaweza kila kitu. Vipo vitu mtu anakuwa haviwezi kabisa ila yupo anakuwa anaviweza vile vitu ambavyo mwenzake haviwezi kabisa.

Sasa wapo watu huwa wanafika mahali wanajitenga na wenzao na kujiona wanaweza kufanya kila kitu wenyewe, ni kweli Mungu wetu ametupa uwezo mkubwa ndani yetu wa kufanya mambo makubwa ila haiwezi kuchukua nafasi ya umhimu wa mtu mwingine.

Umhimu wa mtu mmoja mmoja una maana kubwa katika maisha yetu ya kila siku, iwe kwenye kazi, iwe kwenye biashara, iwe kwenye huduma, kila mtu ana nafasi yake. Akikosekana mtu huyo mwenye nafasi hiyo mambo hayawezi kukaa vizuri.

Unaweza ukawa mwimbaji mzuri sana wa nyimbo za kusifu na kuabudu, au unaweza ukawa mwimbaji mzuri sana wa nyimbo za injili. Ili nyimbo yako ikamilike na kila mmoja aifurahie kuisikiliza, umhitaji mpiga kinanda, unamhitaji mpiga ngoma, unamhitaji mpiga gitaa, unamhitaji mtu anayerekodi sauti za nyimbo zako.

Unamhitaji mtu ambaye atakutengenezea biti, unamhitaji mtu atakayerekodi nyimbo zako kwa video, na mengine mengi yanayofanana na hayo. Ndipo utaona kazi yako inaenda vizuri, ndipo utaona watu wakifurahia kazi yako, na utapata sifa nyingi, na wewe utamrudishia sifa na utukufu Mungu.

Lakini kama ulikuwa unayaweza mambo yote, nafasi hizo zote ulipaswa kusimama mwenyewe, kitu ambacho usingeweza kukifanya kabisa. Lakini pamoja na hayo wapo watu wanafika mahali wanajisahau na kujiona wanaweza kila kitu, wanafika mahali wanaanza kuonyesha dharau kwa watu wengine.

Tuchukulie tu viungo vyetu vya miili yetu, jicho haliwezi kusema sina haja na mkono, jicho kazi yake ni kuona, jicho haliwezi kufanya kazi ya mkono. Hata kama jicho linafanya kazi kubwa sana ya kuona vitu mbalimbali, haliwezi kushika kitu, bado jicho litahitaji msaada wa mkono.

Kichwa nacho hakiwezi kuiambia miguu sina haja na ninyi, pamoja na umhimu mkubwa wa kichwa, miguu nayo ina umhimu wake mkubwa sana. Na miguu haiwezi kuona kichwa hakina kazi kubwa ya kufanya, maana kichwa kikikatwa miguu itakuwa haina kazi.

Rejea: Na jicho haliwezi kuuambia mkono, Sina haja na wewe; wala tena kichwa hakiwezi kuiambia miguu, Sina haja na ninyi. 1 KOR. 12:21 SUV.

Usimwone mwenzako hana kazi ya maana, ukajiona wewe ndio una kazi kubwa kuliko mwenzako, huyo unayemwona ana kazi ndogo na wewe una kazi kubwa. Kabla ya kumtupia lawama nyingi, jiulize yale majukumu ambayo huwa unamwachia ukipewa wewe utayaweza yote?

Utamkuta mtu anamdharau mtu anayefagia barabara, je, huyo mtu anayemdharau anayesafisha barabara ya jiji/mji, jiji/mji huo ungeonekanaje ni safi ikiwa huyu mfagia barabara asingekaa kwenye nafasi yake?

Kila Kiungo kina kazi yake maalum, hata kile unachokiona hakina kazi kubwa, kina kazi kubwa sana japo wewe unakidharau. Mungu alikiweka kwenye eneo hilo ili kiweze kufanya kazi yake vizuri, na ukitaka kujua umhimu wa kiungo hicho, kipate shida yeyote ile utajua umhimu wake baada ya pengo lake kutokea.

Rejea: Na kiungo kimoja kikiumia, viungo vyote huumia nacho, na kiungo kimoja kikitukuzwa, viungo vyote hufurahi pamoja nacho. 1 KOR. 12:26 SUV.

Usidharau nafasi ya mtu, unaweza kufikiri kazi yake ni ndogo sana ila ukiingia kwenye undani utajua huyo mtu ni wa muhimu sana. Hata kama unamwona mtu huyo yupo yupo tu, sio yupo yupo tu, yupo kwenye nafasi yake.

Hapa siwatetei wavivu au wazembe, hapa nasemea huduma/nafasi za watu katika maeneo yao, ambapo nafasi hizo tumezilinganisha na viungo vya mwili wa binadamu.

Binafsi sijawahi kuona kichwa kikigombana na miguu, wala sijawahi kuona mikono inagombana na pua, wala sijawahi kuona masikio yakigombana kichwa. Nimeona kila kiungo kinafanya kazi yake pasipo kutegea chezake, kila kiungo kinawajibika kwa nafasi yake pasipo kuingiliana.

Jifunze hili litakusaidia sana katika maisha yako ya wokovu, usimdharau mwalimu, usimdharau nabii, usimdharau mtume, usimdharau mchungaji, wala usimdharau mwinjilisti. Kila mmoja ana kazi yake katika mwili wa Kristo, Kristo ni mwili nasi ni viungo vyake.

Na kila kiungo kinafanya kazi yake pasipo kuingiliwa na kingine, ukitaka kuanza kuingilia unakuwa unakosea na unaharibu utaratibu wa kiMungu. Na hutoweza kufika mahali kwa kujaribu kuingilia kazi ya kiungo kingine katika mwili wa Kristo.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com