
Mambo mengi mazuri tunayofanya yanakuja kuonekana hayana maana sana kutokana na kuyafanya pasipo utaratibu, jambo lilikuwa zuri sana ila kwa sababu limefanyika pasipo utaratibu linapoteza ule uzuri wake.
Wachache sana wanakuwa wanaelewa kuwa hilo jambo ni zuri ila aliyelifanya ndio ameharibu, wengine wote wanaobaki wanaliona ni baya au wanaliona halina maana yeyote.
Jambo hata liwe zuri sana, usipolifanya kwa uzuri na kwa utaratibu, hilo jambo litaonekana la hovyo, au litaonekana halifai kabisa. Lakini ukija kwenye uhalisia wa jambo lenyewe utaliona ni zuri sana isipokuwa aliyelifanya ndiye aliyeharibu.
Hata katika huduma za kiroho, tunapaswa kuwa makini sana, unaweza ukawa na huduma nzuri sana, usipoifanya kwa uzuri/hekima na kwa utaratibu. Huduma yako itaonekana kero kwa wengine, watu watakuona vingine kabisa na kukosa kitu kizuri kwako cha kujifunza.
Hili linatukwamisha wengi sana hasa wale ambao hatutaki kushauriwa, hasa wale ambao hatutaki kujifunza na kubadilika pale ambapo tunapaswa kubadilika. Utakuta mtu anarudia kosa lile lile kila siku, ukimweleza ukweli anaona unamwonea wivu.
Na ukweli kwamba tunapaswa kupima huduma zetu kwa kupata maoni ya watu, tunapaswa kujua watu wanatuonaje kwa kile tunafanya, na wana ushauri gani ili tuweze kuboresha zaidi. Ndio maana hata Yesu mwenyewe kuna wakati aliwauliza wanafunzi wake kuhusu watu wanamsemaje.
Rejea: Ikawa alipokuwa akisali kwa faragha, wanafunzi wake walikuwapo pamoja naye, akawauliza, Je! Makutano hao wanasema ya kuwa mimi ni nani? LK. 9:18 SUV.
Japo sio kila mtu atakuwa yupo tayari kukuambia ukweli kwa nia njema, wale wachache ambao wanakuwa tayari kukuambia ukweli. Ule ushauri wao huwa tunakuwa tayari kuusikiliza na kufanyia kazi yale ambayo tunaona yana ukweli?
Usijidanganye kwamba huhitaji mtu yeyote wa kukushauri, wala usijidanganye kuwa hakuna mtu anaweza kukufundisha kazi ya Mungu. Ukijiona upo hivyo ujue unaelekea kwenye anguko kubwa, anguko ambalo litakufanya usahaulike.
Na kama ndio ulikuwa unaanza huduma, ujue hutofika mbali, utaendelea kubaki hivyo hivyo bila kupiga hatua zozote. Sababu haswa inakuwa kiburi chako cha kujiona unajua kila kitu huhitaji ushauri wa mtu mwingine.
Rejea: Lakini mambo yote na yatendeke kwa uzuri na kwa utaratibu. 1 KOR. 14:40 SUV.
Unaona hilo andiko linavyosema, kila jambo linapaswa kutendeka kwa uzuri na kwa utaratibu, hii ni hekima ambayo anapaswa kuwa nayo mtumishi wa Mungu.
Usifanye jambo/mambo ilimradi unafanya, fanya kwa uzuri na kwa utaratibu unaoeleweka, sio kwa sababu wewe ni mwimbaji wa siku nyingi unakuwa unalipua mambo. Mambo ya kiMungu hayapo hivyo, wala hupaswi kuleta mazoea, unapaswa kusikiliza ushauri wa wengine. Na unapaswa kumsikiliza Roho Mtakatifu.
Usipofanya hivyo, utashangaa badala ya kuwa baraka kwa watu, unakuwa kero kwa watu, kwa akili yako utadhania hawaelewi kitu. Kumbe wewe unakuwa unafanya mambo sio kwa uzuri na kwa utaratibu unaoeleweka.
Uwe makini sana kwa hili, hasa ukiwa umeokoka na unamtumikia Mungu, hakikisha unafanya mambo ya Mungu kwa uzuri na kwa utaratibu mzuri. Usiende ilimradi unaenda na wakati wewe ni mtu uliye na Roho wa Mungu ndani yako.
Kama bado hujajiunga na kundi letu la wasap la kusoma Neno la Mungu kila siku isipokuwa siku ya jumapili, nakusihi uchukue hatua ya kuwasiliana nasi kwa wasap namba +255759808081 ili uweze kuunganishwa.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com