Mtu kuheshimiwa mahali ambapo ni mgeni, yapo mambo mengi sana huwa yanachangia, lakini leo nizungumzie heshima inayotengenezwa na mwenyeji wako au mtu anayekufahamu vizuri.

Ukiwa kiongozi au ukiwa mchungaji/mtumishi wa kanisa la mahali, una mchango mkubwa sana wa kumtengenezea mtumishi mwenzako aliyekutembelea mazingira mazuri ya kutodharauliwa au kutoonekana vibaya.

Vile vile una mchango mkubwa ukienda kuhudumu kwenye kanisa analochunga mchungaji mwenzako, una nafasi kubwa ya kumsema vizuri mchungaji mwenzako na washirika wake wakaanza kumwona kwa namna ya tofauti kabisa.

Huo ni mfano wa mchungaji, hata wewe ambaye sio mchungaji una nafasi ya kumsema vizuri rafiki yako akapata kibali mahali, bila kufanya hivyo rafiki yako anaweza asipokelewe vizuri na watu. Inaweza kuchukua muda mrefu sana hadi kuja kueleweka na watu kuwa ni mtu mzuri, ambapo huo muda mrefu usingekuwepo kama ungewaeleza watu kuhusu huyo mtu.

Wapo baadhi ya watumishi wa Mungu ambao wametambua hili, wamekuwa baraka kwa watu ambao hawajafahamika sana na kundi kubwa la watu, ambalo wao wanaheshimiwa sana na kundi hilo la watu.

Siku zote unapokuwa na nafasi fulani ya juu katika jamii, jamii ikawa inakufahamu kwa sifa njema, unapomsemea mtu vizuri na ukawaambia wasiwe na shaka naye. Mtu huyo ataishi vizuri sana na atapata ushirikiano wa hali ya juu sana.

Wapo watu wanashindwa kutimiza majukumu yao vizuri, kwa sababu hawakupata mtu wa kuwasemea vizuri, hadi aje atoke kwenye eneo la kudharauliwa, na watu wamwelewe vizuri. Itachukua muda mrefu sana, kwanini achukue mtu mrefu wakati wewe upo, na unaweza kumtengenezea mazingira mazuri.

Hili tunajifunza kwa mtume Paulo, alimsemea vizuri sana Timotheo, kiasi kwamba hata kama kulikuwa na mambo ambayo yangeonekana kumpa shida. Mambo hayo yasingepata nafasi kirahisi, maana aliyemsemea vizuri alikuwa na sifa njema kwa watu wale.

Rejea: Lakini, Timotheo akija, angalieni akae kwenu pasipo hofu; maana anaifanya kazi ya Bwana vile vile kama mimi mwenyewe; basi mtu ye yote asimdharau, lakini msafirisheni kwa amani, ili aje kwangu; maana ninamtazamia pamoja na ndugu zetu. 1 KOR. 16:10‭-‬11 SUV.

Nikupe tahadhari hapa, usije ukawaondoa watu hofu juu ya mtu fulani pasipo kumfahamu vizuri, ukawaambia ni mtu mzuri sana, wasiwe na hofu yeyote naye, bali wampe ushirikiano wowote atakaoutaka kwao.

Ukifanya hivyo bila kumjua vizuri huyo mtu, alafu ikatokea akawafanyia kitendo kisicho sahihi, watu wale watakulaumu wewe. Maana kupitia wewe ndio walimpa ushirikiano na hawakuwa na hofu yeyote kuhusu huyo mtu.

Unaweza kupoteza imani yako kwa watu, au unaweza kupoteza uaminifu wako kwa watu, watakuona na wewe utakuwa miongoni mwa watu wasio wazuri. Kilichowafanya wafikiri hivyo na kukuona tofauti na mwanzo, ni kufanyiwa kitendo kibaya kwa kuwaaminisha wewe ni mtu mzuri.

Jifunze hili utasaidia wengi sana kupata ushirikiano mzuri kwa watu, ukifanya hivyo na wewe utakutana na mazingira fulani magumu. Mungu atakupa mtu wa kukusemea vizuri na watu wakakuelewa vizuri na kukupa ushirikiano wa kutosha.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com