
Sehemu yeyote yenye harufu mbaya, hakuna mtu atatamani kukaa mahali pale, hakuna mtu atasema hapa kuna harufu nzuri. Kila atakayekanyanga mahali pale ataonyesha kukerwa na harufu ile, ataondoka, ama ataziba pua zake.
Harufu mbaya hakuna anayeipenda, nyumba ikiwa na harufu mbaya hakuna mtu anaweza kutamani kukaa pale, labda harufu ile iwe inahusiana na mtu mwenyewe.
Nikiwa na maana kwamba, mtu asiyevuta sigara, kukaa kwa wavuta sigara huku wakivuta sigara zao, hataweza kukabiliana na moshi ule wa sigara. Lakini mtu anayevuta sigara anaweza kukaa pale na asione shida yeyote, maana ile harufu kwake sio tatizo.
Lakini tofauti kabisa na harufu nzuri, kila mmoja atakayeipata harufu yake ataifurahia, maana ni harufu nzuri. Harufu ambayo inavutia kuendelea kuinusa, maana haichoshi pua, maana haikeri, ila inaleta utulivu wa pua.
Ndivyo walivyo wale ambao wameokoka, mtu aliyeokoka anafananishwa na harufu nzuri, manukato mazuri, manukato ambayo yanukia vizuri kwa watu waliomwamini Kristo, na wasiomwamini Kristo, au waliorudi nyuma.
Sio hivyo tu, wale ambao wameokoka ni manukato ya Kristo, mbele za Mungu, miongoni mwa wale wanaookolewa na kwa wale wanaopotea.
Rejea: Kwa maana sisi tu manukato ya Kristo, mbele za Mungu, katika wao wanaookolewa, na katika wao wanaopotea. 2 KOR. 2:15 SUV.
Wewe ni miongoni mwa wale wenye manukato ya Kristo? Wewe ni harufu nzuri mbele za Mungu? Je, wewe ni harufu nzuri kwa wale waliokoka na wale wasiokoka?
Kama si miongoni mwa watu wenye harufu nzuri, unawaza nini? Kwanini usiwe miongoni mwa watu wenye harufu nzuri mbele za Mungu, na wale waliokoka na wasiokoka?
Itakuwa jambo la msingi sana kuwa miongoni mwa watu wenye harufu nzuri, manukato yanayopendwa na kila mtu, ukiwa na harufu nzuri utakuwa kimbilio la wengi. Maana lipo pumziko zuri kwako, watu waliokata tamaa watapata maneno mazuri kwako.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com