
Usipoelewa au usipokuwa makini unaweza kufika mahali ukaanza kujiona nguvu/uwezo ulionao wa kufanya mambo mbalimbali, umetokana na juhudi zako binafsi. Ukaenda mbali zaidi bila juhudi zako usingekuwa hivyo, unaweza ukawa upo sahihi kama hutomwondoa Mungu katika hilo.
Ila kama utamwondoa Mungu katika mafanikio hayo uliyonayo sasa, utakuwa unakosea sana, nguvu na uwezo huo mkubwa ulionao. Umetokana na Mungu, kazi yako ilikuwa kutumia kile Mungu amekupa ndani yako, na sio kwamba umekipata kwa akili zako mwenyewe au si kwamba umekiunda mwenyewe.
Uwezo wa mtu kufundisha Neno la Mungu kwa kiwango fulani kikubwa, anayemfanya aonekane ana viwango vya juu vya kufundisha ni Mungu. Juhudi zingine za mtu kumtafuta Mungu kwa bidii, haziwezi kuondoa nafasi ya Mungu kwa huyo mtu.
Haijalishi mtumishi fulani anatenda miujiza mikubwa ya kiMungu, fahamu kwamba huyo mtumishi anatenda hiyo miujiza si kwa nguvu zake mwenyewe. Bali anatenda hiyo miujiza kwa uwezo wa Mungu ulio ndani yake, huo uwezo ukiondoka ndani yake hawezi kutenda yale anayoyatenda.
Haijalishi mwimbaji fulani anaimba vizuri sana, na anakubalika sana na watu wengi, kibali na uwezo mkubwa alionao wa kuimba hautokani na nguvu zake mwenyewe. Bali uwezo wake unatokana na Mungu, Mungu ndiye anamwezesha kufanya hayo yote.
Chochote unachokiona kwa mtu wa Mungu, kiwe kitu cha tofauti sana na wengine, hicho kitu cha tofauti na wengine hakijatokana na nguvu zake mwenyewe. Kimetokana na uwezo wa Mungu, ndiye anayemfanya anaonekana wa tofauti.
Rejea: Si kwamba twatosha sisi wenyewe kufikiri neno lo lote kwamba ni letu wenyewe, bali utoshelevu wetu watoka kwa Mungu. 2 KOR. 3:5 SUV.
Haleluya, kama ni hivi tunaweza kufika vile viwango tunavyovitaka, maana vyote hivyo vinatoka kwa Mungu mwenyewe, wala havitokani na nguvu zetu wenyewe. Kama kuna mtu anajidanganya hivyo, inawezekana kabisa asifike mbali sana, anguko lake litakuja.
Utoshelevu wetu au uwezo wetu unatoka kwa Mungu, hautoki kwa mwanadamu yeyote yule, kila mmoja unayemwona ana kitu kizuri ndani yake chenye kumletea Mungu sifa na utukufu. Hakitokani na nguvu zake mwenyewe, hicho kitu alichonacho ni kwa uwezo wa Mungu, bila uwezo wa Mungu asingekipata.
Mtu yeyote aliye na bidii mbele za Mungu, anaweza kupewa kile anakihitaji mbele za Mungu, juhudi zingine za kwetu kama wanadamu hizo lazima tuwe nazo ila tukishapata tulichokuwa tunakihitaji. Tusijione tumekipata kwa nguvu zetu wenyewe, tukamsahau Mungu, tukajiona tunaweza kwa nguvu zetu wenyewe pasipo hata Mungu.
Tusifike hatua hiyo, tujue uwezo wa Mungu ulio ndani yetu, tuutambue kabisa uwezo huo wa Mungu ndani yetu, tukishajua hivyo tutaendelea kujinyenyekesha kwa Mungu wetu. Tena tunaendelea kuutafuta uso wake kwa bidii zetu zote.
Tukijua tunayoyafanya si kwa nguvu zetu wenyewe, tutaendelea kulinda uhusiano wetu na Mungu, hatutakubali kuchafua maisha yetu ya wokovu. Bali tutaendelea kuulinda utakatifu wetu, tukijua hatua tuliofika ni kwa uwezo wa Mungu.
Tutajua ubunifu tulionao wa kubuni mambo mapya kila siku, umetokana na Mungu wetu, ukishajua hivyo hutofika mahali ukamkufuru Mungu wako na kujiona ni nguvu zako mwenyewe zinakufanya uwe hivyo.
Usiache kusoma Neno la Mungu, Biblia yako iwe rafiki yako wa karibu sana, siku isipite bila kuisoma. Na kama hili ni changamoto kwako, karibu sana kwenye kundi letu la wasap la kusoma Neno la Mungu kila siku, tuma ujumbe wako wasap namba +255759808081 utaunganishwa.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com