Bila shaka umesikia sana walimu wengi wakishauri uwe msikilizaji zaidi kuliko mwongeaji, yaani ukiwa mahali na wenzako mnajadili mambo mbalimbali. Vyema ukachangua kuwa msikilizaji zaidi kuliko kuwa mwongeaji.

Kama hujawahi kupata kabisa hili somo la kuwa msikilizaji zaidi, na usiwe mwongeaji zaidi, usiwe na shaka leo utaenda kujifunza hili somo na hadi kufikia mwisho utakuwa umejifunza mambo mengi sana ya kukusaidia katika maisha yako.

Wengi huwa tuna tatizo la kuongea sana kuliko kusikiliza, badala yake tumekosa mambo mengi sana katika kupata mambo mazuri kupitia wengine kwa kuchukua nafasi kubwa ya kuongea zaidi kuliko kusikiliza.

Yupo mtu mwingine anaweza akawa anasikiliza mwenzake, kwa kuwa anajua kuna nafasi ya kuja kuuliza maswali. Anakuwa hayupo makini katika kusikiliza, anakuwa bize na mambo yake kichwani, au anajiweka tayari zaidi kwenye kuuliza maswali.

Kumbe yale anayoyaandaa kuja kuuliza maswali, tayari yamejibiwa kwenye mazungumzo, maana yake nini? Huyu mtu hakuwa akimsikiliza mwenzake akiwa anaongea zaidi alikuwa anafanya maandalizi ya kuja kuongea.

Hii tabia sio nzuri kabisa, kusikiliza ni bora zaidi kuliko kuwa mwongeaji, lakini wengi wetu tumekuwa waongeaji zaidi, na watu wa kusikiliza wamekuwa adimu sana.

Unaweza ukawa miongoni mwa watu wachache ambao wanasikiliza zaidi kuliko kuongea sana, kwa sababu katika kusikiliza unajifunza mengi zaidi. Yupo mtu anaongea mbele yako, mpe nafasi ya kuongea, usidakie mazungumzo bila utaratibu, wala usimkatishe katishe, acha amalize kwanza.

Kusikiliza usiache kusikiliza, tena kuwa mwepesi zaidi kwenye kusikia, na kuwa mzito kuongea, sio kana kwamba unajifunza kuwa mzembe, hapana. Muda wako ukifika wa kuongea, utaongea vya kutosha ukiwa tayari kuna vitu umevuna kwenye mazungumzo ya mwenzako.

Rejea: Hayo mnajua, ndugu zangu wapenzi. Basi kila mtu na awe mwepesi wa kusikia, bali si mwepesi wa kusema; wala kukasirika. YAK. 1:19 SUV.

Umeona hilo andiko, linatusihi tuwe wepesi wa kusikia, na si wepesi wa kusema, mtu anayekuwa mwepesi wa kusikia ni mzito kusema. Mara nyingi watu wale huwa makini sana, na wanaweza wakawa na maamzi mazuri.

Umesikia maneno fulani kuhusu mtu fulani, usiwe mwepesi sana wa kusema kabla hujawa na uhakika nayo, ama kabla hujapewa kibali cha kuyazungumza hayo. Kazi yako umesikia, kwenye kusema uwe mzito.

Usikubali kuendeshwa sana na hasira, maana ukiruhusu hasira unakuwa unaongea hovyo, hapa pia unapaswa kufanya hivi unapojikuta unapatwa na hasira.

Kabla ya kutamka neno unapokuwa na hasira, jizuie kwa muda, kisha pima hilo Neno unaloenda kutamka lina maana yeyote au unaenda kuongea neno ambalo halifai. Na linaweza kukushushia heshima yako, ukaonekana mtu asiye na Yesu moyoni.

Zoezi ambalo unapaswa kulifanyia kazi hapa, kuanzia sasa anza kuwa msikilizaji zaidi kuliko mwongeaji, hata kama utakutana na Changamoto katika hili. Usikate tamaa maadam maandiko yanatuelekeza tuwe hivyo, ukifeli siku moja, kesho rudia tena, hadi ufaulu mtihani.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com