Yapo mambo/vitu tukiwa kama watu tuliokoka na kuelimika, huwa tunaona tukivifanya tutaonekana hatujielewi, au tukivifanya tutaonekana hatujakua kiroho, au tukivifanya tutaonekana tunaabudu sana watu.

Wakati tunawaza hayo yote, Je, huwa tupo sahihi? Hili ni jambo la msingi sana kujiuliza na kupata majibu yake sahihi. Bila kupata majibu sahihi au bila kupata maarifa sahihi juu ya hili, tunaweza kuendelea kukosea zaidi au tunaweza kuendelea kufanya kitu bila kuelewa tunachofanya.

Wengi wetu tumekuwa tunachukulia wageni tunaopata kama jambo la kawaida sana, tunapolichukulia hili ni jambo la kawaida. Hata ule ukarimu wa wageni unakuwa mdogo sana, au unakuwa wa kiwango cha chini sana.

Hadi wale wageni wanaotutembelea huwa wanaona labda wamekosea kuja kututembelea, au wengine huwa wanaanza kufikiri wametukosea nini hasa. Kutokana tu na mapokezi yetu, au kutokana na makaribisho yetu hafifu.

Wapo wengine pia huwa wanawajali sana wageni, vile wanawakaribisha na kuwajali, vile wanawakaribisha kwa hofu na kuwatetemekea. Kwa wale ambao hawafanyi hivyo huwaona wanafanya vibaya sana, kitendo cha kuwa na hofu na kuwatetemekea wageni, huwa hakiwapendezi kabisa wao.

Huenda na wewe upo miongoni mwa watu ambao hawapendi wale ambao huwa wanatetemekea sana wageni, leo utaenda kufahamu huwa upo sahihi au huwa haupo sahihi.

Rejea: Na mapenzi yake kwenu yamekuwa mengi kupita kiasi, akumbukapo kutii kwenu ninyi nyote, jinsi mlivyomkaribisha kwa hofu na kutetemeka. 2 KOR. 7:15 SUV.

Ndugu yangu, kumpokea mtu kwa uchangamfu mkubwa na kwa hofu na kutetemeka, kwanza kunamfanya yule unayempokea ajisikie vizuri. Pili sio kitendo ambacho cha mtaani, ni kitendo ambacho kipo kimaandiko, tatu ni jambo ambalo linamfanya mtu huyo mapenzi yake kuongezeka kwa waliompokea.

Huenda hili somo ulilipata kwa wazazi wako, au huenda hili jambo la kuwapokea wageni kwa namna ya hofu na kutetemeka ulilikuta katika jamii yako. Ama ulilikuta kwenye kabila lako linatendeka, au ulijifunza kwa wazazi/walezi wako.

Umeendelea nalo bila kuelewa maana yake ni nini, kuanzia sasa unapaswa kuelewa kuwa ni jambo zuri sana, ambalo linamfanya mtu kujisikia vizuri. Na kuona amejaliwa na watu alioenda kuwatembelea, ikiwa tu hili jambo litatendeka pasipo unafiki.

Kumpokea mtu kwa hofu na kutetemeka nyumbani kwako, au kwenye makusanyiko makubwa, au wakati anashuka uwanja wa ndege, au wakati anashuka stand ya mabasi, au wakati anaingia kanisani, au wakati anaingia kwenye ukumbi fulani. Kama mgeni maalum, tendo hilo ni jema sana, wala sio tendo la utumwa.

Tumeona hapa mtume Paulo anaeleza vile Tito alivyofurahi na kujisikia vizuri baada kupokelewa vizuri, tena alipokelewa kwa hofu na kutetemeka. Kwa Tito kilikuwa ni kitendo cha utii, na mtume Paulo aliona ni jambo zuri.

Kama ulikuwa hufanyi hivyo kwa wageni wanaokutembelea kwa kufikiri ni jambo lisilofaa, kuanzia sasa lione hili jambo linafaa, karimu wageni kwa namna iliyo njema. Utaona baraka nyingi sana zitokanazo na kupokea wageni vizuri.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com