Wakati wa kupanda mema, mara nyingi huwa sio wakati wa kuonekana sana kwa watu wengi, ni wakati ambao mara nyingi huwa huna sifa sana. Ni wakati ambao unakatishwa tamaa sana.

Wakati wa kujitoa sana kwa mambo ya Mungu, wakati wa kujituma sana katika utumishi, wakati wa kuweka bidii katika kusoma Neno la Mungu, ni nyakati ambazo hazionekani sana kwa watu wengi.

Hata kama mtu ataziona, wengi huwa wanazipuuza, wengi huwa hawazingatii sana kile ambacho mtu huyo anakuwa anafanya. Wakati mwingine anaweza kueleweka kivingine kabisa, lakini yule anayefanya anakuwa anavumilia maneno mengi ya watu hao.

Pamoja na kutokuonekana sana nyakati hizo nilizokutajia hapo, pale anapofanikiwa mtu huyo, pale atakapopata matunda makubwa kwa kile alikuwa anafanya, ghafla mtu huyo huanza kupata sifa nyingi sana.

Sifa ambazo siku za mwanzo zilikuwa kejeli kwake, yalikuwa ni maneno ya kuvunja moyo, alionekana kiherehere, alionekana anajipendekeza, alionekana ana shida sana ndio maana anaomba sana, na mengine mengi yanayofanana na hayo.

Ndugu msomaji wangu, unapaswa kuelewa kile kizuri unachopanda kwa wingi kwa watu ndicho utakachovuna kwa wingi, kile kizuri unachopanda kidogo kwa watu ndicho utakachovuna kwa kidogo kilekile.

Vile vile kile kibaya unachowafanyia wengine kwa wingi, ndivyo utakavyovuna matunda ya ubaya ule ule kwa wingi, chochote unachokipanda katika maisha ya watu. Ndicho utakachovuna sawa sawa na ulivyopanda/ulivyotenda kwa wengine.

Rejea: Lakini nasema neno hili, Apandaye haba atavuna haba; apandaye kwa ukarimu atavuna kwa ukarimu. 2 KOR. 9:6 SUV.

Usitarajie mafanikio makubwa, wakati muda unaojitoa kwa kile unafanya ni mdogo sana, vile unajitoa sana muda mwingi kwa kile unafanya. Ndivyo utakavyovuna vingi siku yako ikifika ya kuvuna matunda ya bidii zako.

Ule ubaya wako unaokazana kuwafanyia/kuwatendea wengine kutokana na nafasi uliyonayo sasa, tegemea ipo siku utavuna matunda ya ubaya wako. Haijalishi itachukua muda mrefu sana, amini kabla ya kifo chako utavuna matunda ya ubaya wako uliowatendea wengine siku za nyuma.

Labda utubu mbele za Mungu kabla ya wakati huo wa kuvuna matunda ya ubaya wako hujafika, hapo utakuwa umeokoka adhabu iliyokuwa inakuja mbele yako. Na utakuwa umeepukana na hukumu ya Mungu siku ya mwisho.

Pia tegemea kuvuna matunda ya mema yako uliyotenda, yale mema mengi uliyoyafanya kwa wengine, au uliyoyafanya mbele za Mungu. Siku ya mavuno yako mengi ipo, hata kama utaona imechelewa sana, amini inakuja siku hiyo.

Haya ni mambo tunayojifunza kupitia maandiko matakatifu, vyema ukajenga utaratibu wa kusoma Neno la Mungu kila siku. Ili kuendelea kujifunza mambo mbalimbali yahusuyo maisha yako ya kila siku, ili kama kuna mahali unapaswa kurekebisha, utarekebisha.

Kama bado hujajiunga na darasa letu la kusoma Neno la Mungu kila siku isipokuwa siku ya jpili, tuma ujumbe wako kwa wasap namba 0759808081 utaunganishwa.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com