Wengi wetu matendo yetu tunayajua vizuri sana, hasa tukiwa hatuendi sawa sawa na Neno la Mungu, hasa matendo yetu yakiwa mabaya mbele za Mungu. Tunakuwa tunajua kabisa uhusiano wetu na Mungu haupo vizuri.

Bila kuambiwa na mtu yeyote uhusiano wako mbele za Mungu haupo vizuri, wewe mwenyewe binafsi unakuwa unajua uhusiano wako na Mungu haupo sawa kabisa. Na wachache sana wanakuwa hawajielewi kabisa wapo kundi gani ila walio wengi wanakuwa wanajua uhusiano wao na Mungu haupo vizuri.

Yupo pia anakuwa anajua matendo yake ni safi mbele za Mungu ila anakuwa anataka Mungu mwenyewe amchunguze zaidi kama kuna mahali hayupo sawa. Mungu amrejeshe katika njia yake sahihi au Mungu amjulishe aweze kurejea katika njia sahihi.

Hasa kama ni msomaji mzuri wa Neno la Mungu, yapo mambo mengi utakuwa unajifunza, yapo mambo mengine utakuwa unajiona ulikuwa unafanya. Lakini yalikuwa sio sahihi wewe kufanya, ukishajua hivyo unaweza kutubu mbele za Mungu.

Hii inaonyesha kwamba pamoja na kuokoka kwako bado unapaswa kuendelea kujichunguza sana njia zako mbele za Mungu, kama zipo sawasawa au hazipo sawasawa. Kila wakati unapaswa kujichunguza au kujipima kama upo sawasawa.

Unaweza ukabaki na ukristo wa mazoea, kumbe matendo yako yakawa hayaendani na mtu aliyeokoka, na watumishi wakijaribu kukuambia unakosea unawaona hawajui kitu chochote.

Kupitia andiko hili ninaloenda kukupa hapa chini, utaweza kufahamu kuwa hata sisi ambao tumeshampa maisha yetu Yesu Kristo. Bado tunapaswa kumruhusu Bwana Yesu atuchunguze mioyo yetu, bado tunapaswa kumruhusu Yesu kuyajaribu mawazo yetu kama yapo sawasawa.

Rejea: Ee Mungu, unichunguze, uujue moyo wangu, Unijaribu, uyajue mawazo yangu;   Uone kama iko njia iletayo majuto ndani yangu, Ukaniongoze katika njia ya milele. ZAB. 139:23‭-‬24 SUV.

Je, kabla ya kutaka Mungu akuchunguze moyo wako, umejipima wewe binafsi na kujiona upo sawa mbele za Mungu? Maana yapo mambo mengine unayoyafanya unajua kabisa yanamkosea Mungu wako. Kabla hujataka Mungu akuchunguze moyo wako, tubu kwanza kwa yale ambayo unayafanya sio mazuri.

Mawazo yako kabla hujataka Mungu ayapime kama yapo sawasawa, wewe mwenyewe jifanyie tathimini ujione kama yamekaa sawasawa. Kisha mruhusu Yesu ndani yako ayapime mawazo yako.

Kupitia usomaji wako wa Neno la Mungu unaweza kumruhusu Roho Mtakatifu akuchunguze moyo wako na mawazo yako. Utapata majibu sahihi kupitia Neno la Mungu, utajulishwa njia zako, na utayatambua mawazo yako mabaya kupitia Neno la Mungu.

Na kama huna utaratibu wa kusoma Neno la Mungu kila siku, nakualika katika  darasa letu la kusoma Neno la Mungu kila siku. Tuma ujumbe wako kwa wasapu namba +255759808081 utaunganishwa.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com