Sisi tunaohubiri/tunaofundisha kwa njia ya jumbe za maandishi, mara nyingi watu huwa wanatuchukulia kwa namna ambayo wanaweza wakawaza wao kutokana na jumbe zetu.

Ukiwa mtu wa kukemea dhambi kwa njia ya maandishi, wale wasomaji wako wanaweza kukufananisha na mtu fulani mkubwa sana wa mwili, wengine wanaweza kukufikiria ni mtu fulani usiye na huruma kabisa.

Kila mmoja anaweza kukutafsiri kwa namna anavyokuchukulia kupitia makala zako mbalimbali unazoandika kwenye blog/website, Facebook, Twitter, instagram, na mitandao mingine mingi.

Kwa kuwa hawakuoni ana kwa ana, kwa kuwa hawakufahamu kwa sura, kila mmoja anayekufuatilia kwenye masomo yako mbalimbali. Anaweza kukuchukulia kwa namna yake, kila mmoja anaweza kupata picha ndani yake kutokana na masomo anayoyapata.

Siku anakuja kukuona uso kwa uso, ule mtazamo wake aliokuwa anakuona, anaweza asiamini macho yake, kinachomfanya asiamini ni vile alikuwa anakuwaza kwa namna fulani. Na wakati anakuona kwa macho yake anakuona haupo vile alikuwa anawaza/anafikiri.

Mfano mwingine, mtangazaji wa radio unayemsikiliza sana, alafu ukawa hujawahi kumwona kwa sura, kutokana na sauti yake nzito unaweza kufikiri labda ni mtu mnene sana. Labda kutokana na unajua watu wenye sauti nzito ni wanene, lakini siku unamwona, unakutana na mtu mwenye mwili mdogo.

Mwingine unaweza ukawa unamfikiria atakuwa mwembamba sana kutokana na sauti yake nyembamba, siku unamwona uso kwa uso, unakutana na mtu mwenye mwili mnene sana.

Picha hizi za watu unaowasikiliza kwenye radio au kwa njia ya kusoma makala zao, unaweza ukawatafsiri kwa namna unayoijua wewe. Siku ukaja kuwaona unaweza kuwadharau, au unaweza ukaogopa sana, au unaweza ukamshangaa sana Mungu.

Hili halikuanza kuwepo leo, lilianzia tangu enzi za mtume Paulo, kutokana na nyaraka zake nzito, zilizokuwa zimebeba jumbe kali, na zenye nguvu kubwa kwa kanisa. Wapo waliokuja kumwona kwa sura, walimchukulia kama mtu aliye dhaifu.

Rejea: Maana wasema, Nyaraka zake ni nzito, hodari; bali akiwapo mwenyewe mwilini ni dhaifu, na maneno yake si kitu. Mtu kama huyo na afikiri hivi, ya kwamba jinsi tulivyo kwa maneno katika nyaraka tusipokuwapo, ndivyo tulivyo kwa matendo tukiwapo. 2 KOR. 10:10‭-‬11 SUV.

Hapa yapo mengi sana ya kujifunza ila lililo kubwa hapa, tunapaswa kuwa vile tunahubiri/tunafundisha, iwe tunafundisha kwa njia ya radio, au iwe kwa njia ya maandishi tunayorusha kwenye mitandao mbalimbali. Tunapaswa kuishi maisha yanayompendeza Mungu.

Sio unakemea sana dhambi kwa njia ya jumbe zako, alafu siku watu wanakuja kukuona uso kwa uso, wanakukuta yale ulikuwa unakemea sana ndio maisha yako ya kila siku.

Acha watu wakuone kwa kufikiri ulikuwa mnene sana, au ulikuwa mrefu sana, hiyo sio hoja ya msingi mbele za Mungu, hoja ya msingi ni unaishi maisha matakatifu? Maana wapo watu ni hodari kwa kuandika jumbe zenye nguvu sana na zenye ushawishi mkubwa wa kuwasihi watu waache dhambi, lakini yeye anakuwa anayafanya hayo hayo anayoyakemea.

Mfano, anasema acha uzinzi kwenye makala/jumbe zake nyingi, alafu maisha yake binafsi ni mzinzi kwelikweli, tena yule mzinzi ambaye amevunja ndoa za watu nyingi, tena yule mzinzi ambaye ana sifa mbaya sana mahali anaishi.

Tunapaswa kuishi maisha matakatifu, matendo yetu yanapaswa kuendana na yale ambayo tunayakemea, au yale tunayahimiza watu wengine wanayaishi. Usiwe feki, kuwa halisia, itakuwa ni sifa njema sana mbele za Mungu na mbele za wanadamu.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com