Hili tunaweza kuliona kawaida au tunaweza tusilikumbuke sana kutokana labda hatujui umhimu wake, au huenda hatuna uzito nalo. Lakini kujichunguza wenyewe kama tunaishi katika imani ya Kristo ni muhimu sana kwa kila mmoja wetu.

Tukiwa kama kanisa la Kristo, tunapaswa kuchunguzana kwa kila mmoja wetu kama tunaishi katika imani, kwanini ni muhimu kuchunguzana. Tunaweza tukawa pamoja kama watu waliokoka lakini tusiwe na imani yeyote kwa Bwana Yesu.

Na pasipo imani hatuwezi kumpendeza Mungu wetu, imani ndio nguzo yetu tukiwa wakristo, bila imani kuokoka kwako kutakuwa hakuna maana yeyote. Kama imani ni nguzo yetu muhimu kama wakristo, tunapaswa kujichunguza kila mmoja wetu.

Tunapojichunguza tutajifahamu imani ipo au haipo, hasa tunapokuwa tunapita katika nyakati ngumu katika maisha yetu, je, imani yetu huwa bado ipo kwa Mungu wetu, au huwa inapotea kabisa na kubaki tu watupu ndani yetu?

Kama sio watupu, imani gani huwa tunapanda ndani yetu, huwa inabaki imani ile ile ya Kristo, au huwa inakuja imani nyingine iliyo kinyume na Kristo Yesu. Lazima kujichunguza wenyewe mara kwa mara, ili kujijua kama bado tupo kwenye imani sahihi au imani potovu.

Imani potovu zipo nyingi siku hizi, usipokuwa makini unaweza kujishangaa umehama kwenye imani sahihi ya Yesu Kristo, na kujiingiza kwenye imani isiyo sahihi ya kumpinga/kumkataa Yesu Kristo.

Labda nikuulize mara ya mwisho kujichunguza imani yako ilikuwa lini, ili ujijue kama bado unaishi katika imani ya kweli. Unaweza ukaona ya nini kufanya hivyo ila unapaswa kujua ni jambo la muhimu sana kwa mkristo yeyote mwenye safari ya kwenda mbinguni.

Rejea: Jichunguzeni wenyewe mwone kama mnaishi katika imani. Jipimeni wenyewe. Je, hamtambui ya kuwa Yesu Kristo yumo ndani yenu? Kama sivyo, basi, mmeshindwa kufikia kipimo hicho! 2 Wakorintho 13:5 NEN.

Hata maandiko matakatifu yanatusihi kujichunguza wenyewe tuone kama tunaishi katika imani, hii inaonyesha ni kiasi gani ilivyo muhimu kujichunguza wenyewe tuone kama tunaishi katika imani.

Hupaswi kulichukulia hili jambo kwa kawaida, lipe muda wake mara kwa mara ujipime mwenyewe uone kama unaishi katika imani? Huenda unasema unayo imani kumbe huna, jiangalie na kujipima mwenyewe utajigundua tu.

Tena kupitia usomaji wa Neno la Mungu unaweza kujichunguza vizuri zaidi kwa kujipima na maandiko matakatifu, kama haupo vizuri utajifahamu tu bila hata kuambiwa na mtu. Au inaweza ikatokea mtu akakuambia imani yako haipo sahihi au haipo kabisa kwa Yesu Kristo.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com