Watu wamefika mahali wanashindwa wafuate lipi na waache lipi, yapo mafundisho yanayowaambia wapo kipindi cha neema ya Kristo. Na yapo mafundisho mengine yanayowaambia wanapaswa kushika sheria zote za Musa.

Ukifuatilia mafundisho hayo yote, kila fundisho lina hoja zake za msingi, ukiwa upande wa mafundisho ya neema ya Kristo, unafika mahali unaonekana kuna mambo haupo sawa. Hadi ushike na sheria zote zilizoshuka kwa mkono wa Musa.

Kwahiyo unaweza ukajikuta unahangaika kushika yote kwa pamoja, au ukiwa upande wa kushika sheria zote, unafika mahali unajiona kuna mahali unapelea na unajiona unamkosea Mungu kutokana na kushindwa kushika baadhi ya sheria.

Na ukiwa upande wa mafundisho ya neema ya Kristo, unajikuta unasakamwa na baadhi ya walimu wa sheria za Musa. Ni kama inachanganya hivi ila ndio ukweli wenyewe inachanganya sana wakristo walio wengi.

Mtu anafika mahali anashindwa kuelewa yupo njia sahihi au hayupo njia sahihi, maana kuna wakati anakutana mafundisho ya kumtia moyo kwenye maisha yake ya wokovu. Na kuna wakati anakutana na mafundisho ambayo yanamwonyesha ndani ya moyo wake haendi sawasawa na Neno la Mungu.

Wataabishaji ni akina nani hapa, lazima uwe makini na urejee kwenye maandiko matakatifu ujue yanasemaje kuhusu hili. Huwezi kumjua nabii mtaabishaji kama huna Neno, huwezi kumjua mtume mtaabishaji kama huna Neno, huwezi kumjua mchungaji mtaabishaji kama huna Neno, huwezi kumjua mwalimu mtaabishaji kama huna Neno, na huwezi kumjua mwinjilisti mtaabishaji kama huna Neno.

Hili tunajifunza kwa mtume Paulo, alifika mahali akaona watu wale walioipokea injili ya Kristo ya ukweli, wanageukia injili nyingine ya kushika sheria. Injili ambayo mtume Paulo na wenzake hawakuihubiri kabisa, tena ni Injili ambayo ilikuwa inaonyesha neema ya Kristo haitoshi bila kushika sheria za Musa.

Rejea: Nastaajabu kwa kuwa mnamwacha upesi hivi yeye aliyewaita katika neema ya Kristo, na kugeukia injili ya namna nyingine. Wala si nyingine; lakini wapo watu wawataabishao na kutaka kuigeuza injili ya Kristo. GAL. 1:6‭-‬7 SUV.

Ndugu yangu, uwe makini sana na kundi la wataabishaji katika injili, fahamu kwamba tupo kipindi cha neema ya Kristo, yaani tupo kwenye agano jipya. Unapaswa kuyaelewa vizuri maandiko yanavyosema, bila kuyaelewa utajikuta upo njia panda.

Mtume Paulo akahitimisha kwa kusema yeyote atakayegeuza injili ile ya Kristo waliyoihubiri, awe mtu, au awe malaika kutoka mbinguni. Mtu/malaika huyo alaaniwe.

Rejea: Lakini ijapokuwa sisi au malaika wa mbinguni atawahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo tuliyowahubiri, na alaaniwe. GAL. 1:8 SUV.

Unao uamzi wa kuchagua, uendelee kushika mapokeo potovu ya dini yako, au kugeukia injili sahihi ya Yesu Kristo. Maana tupo agano lililo bora kuliko lile lililopita.

Unao uamzi wa kuondoka kwa wataabishaji, na kwenda mahali sahihi wanapomhubiri Yesu Kristo bila kumchanganya, mahali ambapo wanaisema neema ya Kristo kwa uwazi kabisa.

Neno la Mungu ndio msingi wa mkristo mwenye safari ya kwenda mbinguni, kujiweka pembeni na Biblia yako, au kutokuwa na ratiba ya kusoma Neno la Mungu. Unajikoshesha mambo mengi sana, mambo ambayo yanakufanya uwe mtu wa kutaabishwa na injili mbalimbali zisizo sahihi.

Tenga muda wako kila siku usome Neno la Mungu, bila Neno la Mungu utajikuta huelewi ufuate kipi na uache kipi, au ukafika mahali ukaona kwa Yesu hakufai.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com