
Ndani ya kundi lililokusanyika kwa ajili ya kumwabudu Mungu au lenye nia ya kusikia mafundisho ya neno la Mungu, ambayo wengi wetu tumezoea kuyaita makanisa, ndani ya kanisa/vikundi hivyo kunaweza kuingia watu wenye nia mbaya.
Vikundi vingi vya maombi vilikufa baada ya watu hawa kuingia ndani, walionekana kama wana maombi ila ukweli ni kwamba walikuja kwa nia tofauti kabisa. Na kwa kuwa watu waliwapuuza, walileta mtafaruku mkubwa na kusababisha kundi kusambaa.
Siku hizi vipo vikundi vilivyoungana kwa njia ya mitandao ya kijamii kama vile; WhatsApp, Facebook, instagram, telegram, na mitandao mingine mingi. Vikundi hivi viliungana kwa nia njema kabisa ya kupeana/kushirikishana mafundisho ya neno la Mungu, lakini kwa kutowatambua watu waliojiingiza kwa nia mbaya.
Vikundi hivyo vilikufa kwa sababu ambayo ukiifuatilia unaweza ukaona ni ya kawaida ila chanzo chake haswa ni wale ambao waliingia kwa kazi hiyo maalum ya kuwavuruga watu wa Mungu. Wanaweza wakawa wametumwa, au wanaweza wakawa wametengeneza mpango huo wao wenyewe.
Hili linaweza likawa jambo geni kwako, au unaweza kujiuliza inawezekana vipi watu wenye nia mbaya wakavuruga kundi lenye nia ya kumtukuza Yesu Kristo, au kundi lenye nia ya kumzalia Yesu matunda mema, au kundi lenye kuujenga mwili wa Kristo.
Tunapaswa kuwa macho sana, ukilala kidogo au ukizumbaa kidogo utakuta mmevurugwa na shetani hadi utashangaa ilikuwaje mpaka ikawa hivyo. Na hadi uje ugundue mbaya wako ni nani, tayari kundi litakuwa limesambaa au limeanza kusambaa.
Lakini ukiwa macho ya kiroho, na Neno la Mungu likawa limejaa moyoni mwako utagundua hila za shetani katika kundi lenu, au ukiwa kama kiongozi wa kundi utazitambua hila za shetani haraka sana kabla hajaleta madhara makubwa kwenye kundi.
Hili tunajifunza kupitia andiko hili nitakaloenda kukushirikisha hapa, linatuonyesha wazi kuwa watu wanaweza wakaingizwa kwa siri kwenye kundi lenu. Kuwafuatilia mambo yote mnayofanya, ili waweze kuwaingiza kwenye sehemu ambayo ninyi hamuitaki.
Rejea: Bali kwa ajili ya ndugu za uongo walioingizwa kwa siri; ambao waliingia kwa siri ili kuupeleleza uhuru wetu tulio nao katika Kristo Yesu, ili watutie utumwani. GAL. 2:4 SUV.
Unaona hilo andiko ndugu, unaweza kulichukulia hili kawaida ila fahamu ni mambo ambayo yapo kwenye jamii zetu. Hata kama huelewi sana ila fahamu haya mambo yapo.
Watu wanaweza kutumwa kuja kukuchunguza kwa nia ya kutaka kufahamu mambo yako, kwa jinsi walivyowakarimu na walivyowacheshi unaweza kufikiri umepata marafiki wazuri sana. Bila kufahamu nia yao ni kutaka kujua baadhi ya taarifa zako za ndani.
Hao wote ni Wapelelezi wa mambo ila mi nazungumza wale watu wanaokuja kuwapeleleza, na wakishakujua hamuendi kama wao wanavyotaka muende. Uwe na uhakika watatafuta namna ya kuwavuruga msiwe na umoja wenu.
Na wapo wengine wanaingia kwenye kundi lenu kama watu wenye nia moja na ninyi, kumbe wameingia kwa kazi moja tu ya kuwavuruga msiendelee kuujenga mwili wa Kristo.
Habari njema ni kwamba, ukiwa na Neno la Mungu la kutosha, uwe na uhakika utayatambua mawazo yao potovu. Na ukishayatambua ni rahisi kwako kujikinga nao, au kuwa nao makini, au kuwaondoa kwenye kundi lenu.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com