
Wapo watu wanaopambana usiku na mchana kuhakikisha wanadhoofisha imani ya Kristo ndani ya mioyo ya watu, wanatumia kila njia kuhakikisha watu wanageukia imani nyingine potovu, na kuiacha ile imani ya kweli.
Watu wanaohakikisha jina la Yesu Kristo halitajwi, wanaosimamia upande wa kudhoofisha kabisa ukristo, watu hao wamekuwa kikwazo kikubwa kwa waamini wengi.
Wamewaudhi sana wale ambao wameokoka, yaani wamempokea Yesu Kristo kama Bwana na mwokozi wa maisha yao. Watu wakishamwamini Yesu, alafu akaja mtu ambaye anataka wamwamini mungu mwingine, hapo inakuwa shida nyingine.
Wapo watumishi wanaohubiri injili ya kweli, wameingia kwenye matatizo makubwa baada ya kukutana na watu ambao hawataki kuona watu wakihubiri injili ya Kristo, au hawataki kumwona mtu akihubiri habari za Yesu Kristo.
Siku za leo, au mazingira unayoishi unaweza ukawa hujawahi kukutana na upinzani mkali wa namna hii, au unaweza ukawa hujawahi watu wakipinga kabisa ukristo kwa nguvu zote. Na ukikaa vibaya wanakuua kabisa, sababu haswa ni jina la Yesu.
Zipo nchi ambazo wanajua vizuri sana vile wanapata tabu ya kutangaza habari njema za Yesu Kristo, wakisikiwa wanaweza kuumizwa vibaya sana. Hata wengine wanapoona wenzao wamefanyiwa vibaya waweze kuona hawapaswi kusema habari za Yesu Kristo.
Watu hawa ambao wanakuwa wanapinga vikali injili ya Kristo, watu ambao wapo tayari kuua mtu atakayesimama kwenye imani ya Kristo. Siku Yesu Kristo akiamua kumshughulikia, mtu huyo atakuwa mtu mwema sana.
Rejea: Ila wamesikia tu ya kwamba huyo aliyetuudhi hapo kwanza, sasa anaihubiri imani ile aliyoiharibu zamani. GAL. 1:23 SUV.
Hili tunajifunza kwa mtume Paulo, kabla hajawa mtume Paulo alikuwa na dini yake aliyokuwa anaipenda sana, dini ambayo ilimfanya aue wakristo wengi sana. Mtu ambaye alikuwa tayari kukufanya chochote kibaya kwa mkristo.
Lakini ilipofika wakati, akawa sio Sauli tena anayeua watumishi wa Mungu, bali akawa mtume Paulo. Ambapo amekuja kulifaa kanisa kwa kiwango cha juu sana.
Yesu Kristo hawezi kumwacha mtu yeyote anayewataambisha watu wake wasiwe na furaha, siku yake ikifika Bwana atamshughulikia huyo mtu anayelitesa kanisa lake.
Haya tunajifunza kupitia maandiko matakatifu, na uzuri wake maarifa yote yanapatikana ndani ya Neno la Mungu. Hakikisha unasoma Biblia yako kwa mpangilio mzuri, na umwombe Roho Mtakatifu akusaidie kuelewa maandiko matakatifu.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com