
Ukiwa kama mtumishi wa Mungu wa kweli au ukiwa kama mtu aliyeokoka sawasawa, kuusema ukweli kwako linaweza likawa jambo la kawaida kabisa kwako. Bila kujalisha wangapi wataupokea, na wangapi wataupinga huo ukweli.
Kuusema ukweli kuna gharama yake kubwa, kuusema ukweli kunaweza kuhatarisha uhai wako, ukweli unaweza kukufanya ukachukiwa sana na wale ambao unawaambia ukweli.
Usipokuwa makini unaweza ukawa mkristo, na watu wakawa wanajua hivyo kuwa wewe ni mkristo mwaminifu mbele za Mungu ila ukawa muoga wa kuusema ukweli.
Kinachokufanya uwe muoga usiuseme ukweli ni kule kukwepa lawama, kule kukwepa kutengwa na marafiki, kule kukwepa kuonekana umeokoka sana kuliko wengine.
Mtu akishaona hivyo anaweza akawa kimya kwa mambo ambayo alipaswa kukemea, au alipaswa kuonya, kinachomfanya awe mkimya ni kuepuka lawama za watu ambao hawataki kuona wanaambiwa ukweli.
Watu ambao hawataki kuambiwa ukweli ni wale ambao maisha yao ya wokovu si mazuri, wanaweza wakawa wakristo kweli ila matendo yao yakawa hayampendezi Mungu. Pale unapojaribu kuwaeleza ukweli wanakuwa wanaona unawafuatilia maisha yao.
Kuwa adui kwa wale unaowaeleza ukweli wa Mungu haujaanza leo, wala hujaanza kwako, hili limeanza tangu zamani, tunalithibitisha kutoka kwa mtume Paulo. Anahoji kuhusu hili la kuusema ukweli;
Rejea: Je! Nimekuwa adui wenu kwa sababu nawaambia yaliyo kweli? GAL. 4:16 SUV.
Huenda hapo ulipo sasa unapitia hali fulani ya kutengwa na marafiki zako, au na ndugu zako, au na wafanyakazi wenzako, au na washirika wenzako, au na majirani zako. Fahamu/jua kwamba haijaanzia kwako, tangu zamani hali hii ilikuwepo.
Usije ukaacha kuusema ukweli, ukweli unaotokana na Neno la Mungu, ukweli usio na unafiki ndani yake, ukweli wenye nia ya kumsaidia mtu akae kwenye mstari ulionyooka. Maana sio wote wanaokuambia ukweli wanakuwa na nia njema ndani yao, wengine wanakuwa na sababu zao maalum.
Je, wewe ni mtu unayeisema kweli ya Kristo bila kujalisha wangapi watakuchukia? Jibu la swali hili naomba ujipe mwenyewe bila kujipendelea. Kama huwa husemi ukweli jipe jibu hilo, na kama huwa unasema kweli bila kuangalia ukaribu ulionao na hao watu, napo jipe majibu sahihi bila kujipendelea.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com