
Kwa kuwa hatupo chini ya sheria tena baada ya Yesu kututoa huko, haimaanisha kwamba kwa sababu tupo huru ndani ya Yesu Kristo, basi tufanye chochote tunachojisikia kufanya.
Huo uhuru ambao unatakiwa kuwepo kwa mkristo yeyote, pamoja na tupo huru, hatuwezi kunywa pombe, hatuwezi kufanya uasherati/uzinzi, hatuwezi kutukana watu hovyo, hatuwezi kufanya chochote kile kichafu tunachojisikia.
Rejea: Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu. GAL. 5:19-21 SUV.
Unaona hilo andiko linavyosema, ukisema wewe upo ndani ya Yesu Kristo, ukajiona upo kwenye neema ya Kristo, usije ukajiona upo uhuru kufanya unachojisikia kufanya.
Pamoja na upo huru ndani ya Yesu Kristo, Usiruhusu tamaa zako za mwili zianze kukutawala ndani yako, ukiziacha zikutawale ndani yako, maana yake mbinguni hutoingia.
Uhuru wetu ndani ya Kristo sio kuturuhusu tufanye chochote, la hasha, uhuru wetu una mipaka, ndio maana unapaswa kujilinda sana na mambo mabaya. Unapaswa kulinda sana moyo wako, kama maandiko yanavyosema linda sana moyo wako.
Rejea: Linda moyo wako kuliko yote uyalindayo; Maana ndiko zitokako chemchemi za uzima. Mithali 4:23.
Kama tunasisitizwa kulinda sana mioyo yetu, uhuru wetu wa kufanya kila tunachotaka unatoka wapi? Utaona uhuru unaozungumzwa hapa sio uhuru wa kufanya mambo yasiyofaa mbele za Mungu.
Usije ukachukulia uhuru wetu ndani ya Kristo, ukaona ni fursa kwetu kufanya chochote kile ambacho miili yetu inawaka nacho tamaa. Hiyo haipo, lazima ujipe mipaka, au lazima uwe na mipaka ukiwa mtu aliyeokoka sawasawa.
Hupaswi kujiachia hovyo kwa sababu upo huru ndani ya Yesu, uhuru wako ndani ya Yesu, sio tiketi ya wewe kufuata tamaa za mwili. Maana mwili huwa upo kinyume kabisa na mapenzi ya Mungu.
Hili ninalokuambia hapa, tunatahadharishwa kupitia andiko hili hapa chini ninaloenda kukushirikisha, maana unaweza kufikiri upo huru kufanya unachojisikia kufanya.
Rejea: Ndugu zangu, ninyi mliitwa ili mwe huru, hivyo msitumie uhuru wenu kama fursa ya kufuata tamaa za mwili, bali tumikianeni ninyi kwa ninyi kwa upendo. Wagalatia 5:13 NEN.
Nimeona Biblia ya neno umeuweka vizuri zaidi huu mstari, kwa kiswahili kinachoweza kueleweka kirahisi kutokana na nyakati tulizonazo sana. Unaona vile uhuru wetu hauwezi kutufanya tukafanya tunachojisikia.
Kama ulikuwa unafikiri upo huru kufanya unachojisikia, kuanzia sasa ondoka kwenye mawazo hayo potovu, Usiutumie vibaya uhuru wako ukakupeleka jehanamu. Tumia uhuru wako kumwabudu Mungu wako vizuri, bila kuwekewa sheria ngumu za kutuzuia.
Hapa ndipo umhimu wa kusoma Neno la Mungu unapoonekana kwa mkristo yeyote mwenye safari ya kwenda mbinguni, kama kweli una tamani kuingia mbinguni. Lazima ukae katika njia sahihi unayoelekezwa na Neno la Mungu.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com