Unaweza ukawa unajiona upo vizuri kimwili, una mali za kutosha, una kazi nzuri, una elimu ya kutosha, una chochote kile kizuri kwako. Kama hujaokoka na unaendelea kumtenda Mungu dhambi, katika ulimwengu wa roho wewe ni mfu.

Inaweza ikawa ngumu kwako kulipokea/kulikubali hili jambo kwa haraka ila unachopaswa kufahamu ni kwamba umekufa, ila inawezekana ukafufuliwa tena kiroho. Kule kuamua kuachana na mambo machafu ya dunia, na kuamua kuokoka, kitendo hicho kinakufanya uwe hai tena.

Yesu Kristo alikuja kutukomboa wanadamu wote ila sharti ulikiri jina lake, bila kulikiri jina lake, Shetani ataendelea kukutumikisha, mbaya zaidi unaonekana umekufa. Hata kama unajiona mzima kwa nje, kwa upande wa kiroho wewe ni mfu.

Rejea: Nanyi mlikuwa wafu kwa sababu ya makosa na dhambi zenu; ambazo mliziendea zamani kwa kuifuata kawaida ya ulimwengu huu, na kwa kumfuata mfalme wa uwezo wa anga, roho yule atendaye kazi sasa katika wana wa kuasi. EFE. 2:1‭-‬2 SUV.

Dhambi zako/zetu ndio zinatufanya tuonekane tumekufa, uhai wetu wa maisha ya kiroho ni kuishi maisha safi mbele za Mungu. Nje na hapo tutaendelea kujiona tupo vizuri ila mbele za Mungu tupo vibaya.

Inawezekana kabisa ulimkiri Kristo, na inawezekana unasali kila jumapili, kama unatenda dhambi, fahamu kwamba umekufa kiroho, tena umeua uhusiano wako na Yesu Kristo.

Ikiwa uhusiano wako na Yesu Kristo umekufa kwa sababu ya dhambi zako, unayo nafasi ya kugeuka sasa, unayo nafasi ya kumgeukia yeye na ukamwomba msamaha, yaani ukatubu mbele zake.

Ukishatengeneza na Bwana Yesu, utaona dhamiri yako ikikushuhudia kwa uwazi kabisa kuwa uhusiano wako na Mungu umerejea upya. Hii ni baada ya kumrudia kwa toba, na ukishatubu hupaswi kuendelea na dhambi.

Hakikisha upo hai kiroho na kimwili, usiwe hai kimwili katika kioo cha Mungu unaonekana umekufa/mfu, uwe hai kiroho na kimwili katika jina la Yesu Kristo aliye hai.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com