Kufikia kusudi la maono yako sio jambo rahisi kabisa, ama kuendelea kushikilia maono yako uliyopewa na Mungu sio jambo jepesi hata kidogo. Vipo vizuizi vingi sana utakutana navyo njiani, haijalishi Mungu amekupa hayo maono uliyonayo.

Wengi wetu tukishakutana na changamoto ngumu katika safari yetu, huwa tunaanza kuona hayakuwa maono ya Mungu. Mbaya zaidi uwe huna Neno la Mungu moyoni mwako, unaweza kuvunjika moyo na kukatisha safari yako.

Kukatishwa tamaa ni rahisi sana kama utakuwa huna Neno la Mungu la kutosha moyoni mwako, ukikutana na watu ambao na wao mioyoni mwao hawana Yesu Kristo, au wanaye ila hawajui kitu Mungu alichokupa ndani yako.

Tukitazama maisha ya Yusuf, tangu siku ile Mungu alivyomwotesha ndoto ya kuja kutawala, aliingia kwenye vita ngumu sana, vita iliyoanzia kwa ndugu zake. Hadi akajikuta yupo utumwani, na huko utumwani napo aliendelea kukutana na majaribu magumu(kunusurika kubakwa na kufungwa gerezani).

Pamoja na ugumu aliokuwa anakutana nao, Yusuf bado alikuwa amesimama na Mungu wake, na mwisho tunaona ndoto yake ilitimia huko Misri. Hadi kufika hatua kuitwa waziri mkuu, haikuwa rahisi, japo Mungu alishamkusudia awe hivyo.

Yusuf hakumwasi Mungu wake, lakini leo sio ajabu ukamkuta mtu amesharudi nyuma kabisa kwa sababu ya changamoto ngumu alizokutana nazo kwenye maisha yake ya ujana.

Wapo watu walikuwa waimbaji wazuri ila wameasi maono yao, wapo watu walikuwa walimu wazuri sana wa Neno la Mungu ila leo wameasi maono yao, wapo watu walikuwa wainjilisti wazuri sana ila leo wameasi maono yao.

Kitu gani kilichowafanya wayaasi maono yao? Ni kule kukosa tunda la Uvumilivu, ni kule kudanganywa na shetani na kujiona haikuwa Mungu kuwapa maono hayo. Lakini ndani yao dhamiri zao zinawashitaki kwa kuacha kile walikuwa wanafanya.

Mtume Paul anatupa somo lingine kubwa, yeye anasema hakuyaasi yale maono ya mbinguni. Pamoja na misukosuko yote aliyokutana nayo kwenye huduma ya injili, mtume Paulo hakuyaasi maono ya mbinguni.

Rejea: Kwa hiyo, Ee Mfalme Agripa, sikuyaasi yale maono ya mbinguni. MDO 26:19 SUV.

Ndugu yangu kama unasoma ujumbe huu na ulishaasha huduma aliyokuitia Yesu Kristo, Rudi magotini utubu dhambi hiyo. Hupaswi kuyaasi maono ya mbinguni, hata kama vita vikiinuka vikali sana juu yako.

Kama umefika mahali ambapo unaona kufikia hatima ya maono yako itakuwa ngumu kutokana na changamoto ngumu unazokutana nazo kwenye maisha yako. Nikutie moyo kuwa usikubali kurudishwa nyuma na jambo lolote, endelea kusonga mbele na kumwamini Yesu Kristo.

Kataa roho ya kuyaasi maono ya mbinguni, Mungu alikupa hayo maono akijua unao uwezo wa kuyatimiza, endelea kuimarika katika Kristo. Usiyumbishwe na chochote hadi ufikie hatima ya maono yako.

Hakikisha Neno la Mungu ndio chakula chako cha kiroho, nikiwa na maana usikubali siku ipite bila kulisha roho yako Neno la Mungu. Haijalishi unapitia hali gani ngumu katika maisha yako, Neno la Mungu liwe sehemu ya maisha yako.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com