Wapo watu ambao Mungu amewapa neema ya kuwa mfano bora kwa wengine, yaani wanakuwa nuru kwa wengine ambao hawajamjua vizuri Kristo. Kupitia wao wanakuwa wanajifunza vitu vya msingi kupitia mafundisho yao wanayotoa, na mafundisho hayo yanakuwa kama ufunguo wa watu wale.

Wapo pia watumishi ambao Mungu anawatumia kwa kiwango cha juu sana katika utumishi wao, wale watumishi wadogo wanaoanza kuchipukia katika huduma. Wale watumishi ambao Mungu amewainua, hutumika daraja la wale chipukizi kujifunza mambo ya msingi ya kuwasaidia katika utumishi wao.

Inapofika mahali wale watu au wale watumishi wanaotumika kama mfano wa kuigwa, au wanaotumika kuwapa mafundisho sahihi ya Neno la Mungu ya kuwasaidia kufikia hatima ya wito wao.

Wakaanza kupata matatizo yasiyokoma, ule utumishi wao ukawa unaandamwa sana na shetani kwa jinsi ambayo inawagusa na wale ambao walikuwa wanachota maarifa muhimu kutoka kwao.

Uwe na uhakika, mambo magumu yanayowapata watu wale ambao Mungu anawatumia kwa kiwango cha juu, yatakuwa yanawagusa kundi nzima ambalo lilikuwa linategemea kupata maarifa sahihi kutoka kwao.

Tunajua kwamba mchungaji anapopigwa na kondoo wake aliokuwa anawachunga watasambaratika, hili ni jambo ambalo linaingia kila eneo ambalo lina kiongozi imara. Kiongozi akipatwa na shida, uwe na uhakika na kundi lake lipata shida.

Sasa tunapoona wale watumishi ambao tulikuwa tunajifunza kupitia kwao, au walikuwa wanatuongoza katika njia sahihi, tunapaswa kuwaombea sana. Ili pale wanapokutana na shida, waweze kuvuka salama na kurudi katika hali zao nzuri.

Kinyume cha hayo, wapo watumishi huwa wanageuka faraja kwa wale ambao alikuwa nao karibu wanapovunjika moyo, yeye hugeuka sababu ya kuwatia moyo. Ambapo kwa kawaida tulitarajia yeye ndiyo atiwe moyo katika dhiki au mateso anayopitia wakati huo.

Hili tunajifunza kwa mtume Paulo, anawatia moyo wafuasi wake, jambo ambalo sio la kawaida, hili linaonyesha ni jinsi gani kiongozi anavyopaswa kuwa kwa sura nyingine.

Rejea: Basi naomba msikate tamaa kwa sababu ya dhiki zangu kwa ajili yenu, zilizo utukufu kwenu. EFE. 3:13 SUV.

Hichi kitendo kinaweza kisiwezekane kwa mtu ambaye hajaokoka, isipokuwa kinawezekana kwa mtu aliyeokoka na akawa ana Neno la Mungu la kutosha moyoni mwake. Mtu huyu anaweza kugeuka faraja kwa wale watu wanaomtazama yeye.

Sawa na mzazi anawaambia watoto wake, msikate tamaa mnavyoniona nateseka hivi, hii ni kwa ajili ya faida yenu wenyewe. Hapa watoto na wao wanapaswa wawe na ufahamu wa kuelewa mambo, nje na hapo wataendelea kuteseka ndani ya mioyo yao.

Nami nakuambia usikate tamaa pale unapoona yule ambaye alikuwa kama dira yako, unamwona anapitia mambo magumu, usianze kuona kila kitu kwako kimefika mwisho. Jambo unaloweza kufanya kwake ni kumwombea Mungu, na kufanya kile kilicho ndani ya uwezo wako, nje na hapo utajitesa bure.

Kumbuka kusoma Neno la Mungu(Biblia yako) ni jambo la muhimu sana sana kama mkristo mwenye safari ya kwenda mbinguni, hili sio jambo la kufikiri sana. Unapaswa kuchukua hatua ya kusoma Neno la Mungu haraka iwezekanavyo, kama unapenda tuwe pamoja katika hili tuwasiliane kwa wasap namba +255759808081.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com