Kama kuna kitu kitawakosesha mbingu wake wengi walio ndani ya ndoa, ni kukosa utii kwa waume zao, hichi kitu kama vile kimeanza kuonekana kitu cha kawaida kwa Wanawake wengi ila siku parapanda ikilia wengi hawatanyakuliwa.

Shida iliopo sasa kwa Wanawake wengi waliopo kwenye ndoa, akiwa na shughuli au akiwa na kazi nzuri au akiwa na biashara zake kubwa. Zinazoingiza fedha za kutosha, anajiona na yeye ni mwanaume ndani ya nyumba.

Hataki tena kumtii mume wake, anataka kufanya anachotaka yeye, yaani ndani ya nyumba anataka yeye asiingiliwe na mume wake kwenye maamzi yake. Kisa yeye ana fedha za kutosha, anaona amemaliza kila kitu.

Mbaya zaidi mwanamke huyu awe amemdhidi mume wake kipato, anataka awe anaamua chochote anachotaka yeye, anaweza kuamua leo anakuja nyumbani saa fulani, anaweza akaamua kesho ataenda mkoa fulani au nchi fulani. Bila hata kuomba ruhusa kwa mume wake.

Pesa ni jawabu la mambo yote ila pesa hiyo hiyo haiwezi kuchukua nafasi ya mwanaume, maadam ni mume wako, nafasi yake haiwezi kuzibwa na kitu chochote. Kama kweli umeokoka na Yesu Kristo yupo ndani yako, huwezi kuacha kumtii mume wako.

Kumtii mume ni agizo la kila mwanamke aliye ndani ya ndoa, mwanamke atakayevunja hili na kutaka asimame kama mwanaume, ama kumwona mwanaume ni takataka kwake. Maana anajua anaweza kupata mwanaume yeyote anayemtaka yeye, basi huyo mwanamke Kristo hayumo ndani yake.

Rejea: Enyi wake, watiini waume zenu kama kumtii Bwana wetu. Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe, kama Kristo naye ni kichwa cha Kanisa; naye ni mwokozi wa mwili. EFE. 5:22‭-‬23 SUV.

Utasema wanaume wengine ni wakorofi sana, lakini Ukifuatilia ukorofi mwingi umeanzishwa na wake wenyewe, tabia hii hii ya kutotaka kumtii mume wake. Ndio inaibua mambo mengi ambayo yanakuwa kama yametoa nafasi ya wao kutengana.

Wake wengi ambao hawatambui nafasi ya mume kama kichwa, wameleta shida kubwa kwenye ndoa zao, chanzo kikuu wakiwa wao wenyewe ila hilo huwa walitambui haraka.

Unakuta mwanamke anatoa mambo ya ndani ya mume wake, mwanamke huyo huyo hana utii kwa mume wake, alafu anategemea ndoa yake iwe na utulivu. Kitu ambacho hakiwezekani kabisa, wakati maandiko yanatoa mwelekeo wa hili.

Rejea: …wala mke asikose kumstahi mumewe. EFE. 5:33(b) SUV.

Mwanamke akikosa kumtii mume wake, hata kumstahi hataweza, ndio yale utakuta mwanamke analalamika huko nje nina “mwanaume gani huyu.” Anashindwa kuelewa kuwa alimpenda mwenyewe na akakubali kuolewa naye kwa hiari yake.

Na mwanaume huyu sio kana kwamba ni mkorofi, na sio kana kwamba anafanya mambo mabaya, hapana, isipokuwa mwanamke huyu amemdhidi mume wake kipato, basi anajiona yeye ndio yeye.

Utasema mambo ya kunyenyekeana huo ni mfumo dume, uzuri wake sio mimi niliyesema kuhusu kuwatii wanaume zetu, bali ni maandiko yenyewe yanazungumza kwa uwazi kabisa.

Mume wako ni kichwa, hata kama hupendi kusikia hivyo, fahamu hivyo, na huwezi kugeuza hilo, na kama humtii mume wako, unakosea sana na unajikosesha baraka za Mungu.

Lifahamu Neno la Mungu likusaidie katika maisha yako ya ndoa, usiache nafasi kubwa ya kujaza maarifa ya dunia hii kuliko Neno la Mungu. Ili ndoa yako iwe salama, Neno la Mungu ni muhimu kujaa moyoni mwako.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com