
Inawezekana unakula vizuri sana, unafuata kanuni zote za ulaji wa vyakula vile umeshauriwa na daktari, katika hili la chakula umefanikiwa vya kutosha. Na moyoni mwako unaona upo vizuri katika eneo hilo la chakula, unajua ni chakula kipi ule, na unajua chakula kipi hupaswi kula.
Ukija kwenye mazoezi ya mwili wako, umehakikisha ratiba yako ya kufanya mazoezi ya mwili/viungo huivunji kwa namna yeyote ile. Umekuwa makini katika hilo la mazoezi na unaona afya yako ipo vizuri sana, na ukiangalia mwili wako vile ulivyojijenga kwa mazoezi, unajisikia vizuri sana.
Ukija kwenye eneo la kuangalia afya ya mwili wako baada ya miezi kadhaa uliyoshauriwa na daktari wako, unalifanya hilo kwa uaminifu mkubwa sana. Na unafahamu mambo mengi kuhusu afya ya mwili wako kutokana na vipimo mbalimbali unavyofanya mara kwa mara.
Kama ni maji ya kunywa unajua ni kiasi gani unapaswa kunywa kwa siku, na hili upo nalo makini kutokana na vile daktari alikushauri unywe maji ya kutosha. Hili kwako sio shida tena maana imekuwa kama sehemu yako ya maisha kunywa maji ya kutosha kwa kipimo ulichoambiwa.
Tukija kwenye mazingira ya kulala kwako, umetengeneza mazingira mazuri sana ya kulala na familia yako au wewe mwenyewe. Kama ni usingizi unapata ulio mzuri na mazingira mazuri kiafya, hilo halina shida kabisa kwako.
Pamoja na hayo mazuri yote, kuna mahali unakosea, usipopashughulikia haraka itakuletea shida, maana tayari umejipunguzia mwenyewe miaka ya kuishi kwako. Unafanya kila kitu kuhakikisha upo salama ila kuna mahali unakosea sana.
Mahali penyewe unapokosea na kujipunguzia miaka ya kuishi kwako hapa duniani ni kutowaheshimu wazazi wako, kukosa kwako heshima kwa wazazi wako. Umekosa u heri wa kuishi siku nyingi hapa duniani.
Rejea: Waheshimu baba yako na mama yako; amri hii ndiyo amri ya kwanza yenye ahadi, Upate heri, ukae siku nyingi katika dunia. EFE. 6:2-3 SUV.
Kama nilivyotangulia kusema hapo juu, huenda umejitahidi sana kujiweka vizuri sana kwenye maeneo yale muhimu ya kukufanya afya yako iendelee kubaki salama. Lakini maandiko yanatuambia hapo, ili upate heri ya kuishi siku nyingi hapa duniani, unapaswa kuwaheshimu wazazi wako.
Kama huna heshima kwa wazazi wako, huna muda nao, unawaona kama watu wasio na umhimu sana kwako, upo bize na mambo yako. Huenda wapo mbali na wewe, na unasikia wanaumwa sana ila husukumwi hata kuwapatia fedha kwa ajili ya matibabu.
Sio kana kwamba huna fedha za kuwapa, fedha unazo ila unaona haina sana haja ya kufanya hivyo, nikuambie tu ndugu yangu kujihangaisha kwako kujiweka vizuri ni bure, hakuna maana yeyote.
Kifo kipo kwa kila mtu ila wewe unajitakia mwenyewe kama huwaheshimu wazazi wako, kitendo cha kutowaheshimu tu wazazi wako. Kinakufanya upunguziwe hesabu ya miaka yako ya kuishi, kama Mungu alipanga uishi miaka 80, unaweza ukaishi pungufu ya hapo kwa kukosa kwako heshima kwa wazazi wako.
Kama unasoma ujumbe huu na uhusiano wako na wazazi haupo vizuri, kwa kukosa kwako heshima kwao, tubu haraka kwa kwenda kuwaomba msamaha na kutengeneza pale ambapo hapakuwa sawa.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com