
Kama wakristo, jamii isiyomjua Kristo inapaswa kutusoma kwa sifa njema, sifa ambazo zinaweza kuwavuta hata wao wakaona kuokoka ni kuzuri sana. Hata kama wasipokuambia moja kwa moja ila wanakuwa wanakusema vizuri.
Tofauti kabisa na siku za leo, baadhi ya watu wanaosema wameokoka wanasomeka vibaya, sifa zao hazifanani na mtu aliyeokoka sawasawa. Utakuta amejaa lawama nyingi, sio kana kwamba anasingiziwa ila ni ukweli.
Udanganyifu umekuwa sifa mbaya kwa waamini wengi, mtu haoni aibu kuongea uongo, mtu haoni aibu kufanya udanganyifu wa wazi kabisa. Hata wale wasioamini wanakuwa wanashindwa kujitofautisha naye, tena wanakuwa wanaona haina haja kuokoka.
Tunapaswa kuwa watu ambao matendo yetu yanamtangaza Yesu Kristo kwa sifa njema, watu tunaoamika kwa jamii, watu ambao wanatumiwa na wale wasioamini.
Rejea: Mpate kuwa wana wa Mungu wasio na lawama, wala udanganyifu, wasio na ila kati ya kizazi chenye ukaidi, kilichopotoka; ambao kati ya hao mnaonekana kuwa kama mianga katika ulimwengu. FLP. 2:15 SUV.
Unaona hilo andiko, linatukumbusha au linatutaka tuwe watu wazuri, tuwe watu waaminifu, watu ambao tunaweza kupewa mali ya mtu mwingine. Bila mwenye mali kuwa na hofu yeyote ya kuiba sehemu fulani ya mali yake.
Watu ambao tukiazimwa pesa, tunarudisha bila usumbufu wowote, bila kumkataa yule aliyetukopesha pesa zake. Maana wapo watu wakishakopeshwa pesa za watu, nia yao wanakuwa kuwadhulumu wale waliowakopesha pesa zao.
Na wakiona wanafuatiliwa sana, huwageuka na kuwaambia wale waliowakopesha wana ushahidi gani wakati wanawakopesha, sasa unakuta walipewa tu msaada bila masharti yeyote.
Wengine wanafika mahali wanakuwa wanasema hawapo kabisa au wamesafiri, kumbe wapo ila hawataki kulipa madeni ya watu, au wengine wanakuwa wanatishia wengine uhai. Utafikiri hakupewa au hakuazimwa pesa na huyo anayemtishia uhai wake.

Unapaswa kujihoji sana, maisha yako ya wokovu yanasomekaje na watu, hasa wale wasioamini wanakufahamu kwa sifa njema au mbaya? Kama unafahamika kwa utapeli au kwa udanganyifu, kuanzia sasa rekebisha hilo kwa kutubu mbele za Mungu.
Tuliokoka tunapaswa kuwa mwanga wa kuwaongoza wengine wasiomjua Yesu Kristo, waweze kumkiri kama Bwana na mwokozi wao. Hata kama hawatajua mengi ila kupitia uaminifu wetu kwao, wakiri kwa vinywa vyao kuwa tunaye Mungu wa kweli.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com