
Katika maeneo ambayo hutakiwi kuleta sana mazoea ya kupitiliza au kutumia uzoefu wa kibinadamu bila kumsikiliza Roho Mtakatifu, ni baada ya kuokoka. Unapookoka hupaswi kuwa na mazoea sana kwenye maeneo yale muhimu ambayo yatakufanya uendelee kuonekana mwana wa Mungu.
Yapo mazingira tunapaswa kuwa na tahadhari nayo, haijalishi tunajiona tupo vizuri sana kiroho, haijalishi uhusiano wetu na Mungu upo vizuri sana. Tunapaswa kujihadhari sana na watu wenye matendo mabaya, bila kujalisha tupo vizuri kiroho, tahadhari ni muhimu sana.
Kwanini tunapaswa kuwa na tahadhari? Kwa sababu tusipokuwa makini tutajikuta na sisi tumekuwa kama wao, au tutajikuta tumeanza kushirikiana nao kwa yale mabaya yanayomuudhi Mungu.
Sasa mwingine anaweza kusema ya nini niwe na tahadhari na mtu ambaye hajaokoka, au na mtu ambaye anatenda mambo mabaya, anajiuliza hivi kwa sababu anaona yupo vizuri na Mungu.
Pamoja na kuwa vizuri na Mungu wako, tahadhari ni muhimu sana, bila tahadhari utajikuta umeingia kwenye mtego wa shetani, na kutoka kwenye mtego huo itakuhitaji Mungu akusaidie. Ama utajikuta umeingia kwenye aibu kubwa ya jina la Yesu kutukanwa kwa ajili yako, maana mazingira utakayokutwa nayo ni ya aibu.
Kuokoka sio kigezo cha kujiachia unavyotaka, unapaswa kuwa na tahadhari kila eneo unapokuwa na watu wasiomjua Yesu Kristo au wanaomjua ila matendo yao hayaendani na kusema kwao wameokoka.
Rejea: Jihadharini na mbwa, jihadharini na watendao mabaya, jihadharini na wajikatao. FLP. 3:2 SUV.
Jihadhari ndugu, huu ndio ujumbe wa leo, wengi wamerudi nyuma kiimani kwa sababu hawakujihadhari, wakajikuta wamemwacha Mungu na kutenda mambo yasiyofaa.

Walipokuja kushtuka tayari walishakuwa eneo ambalo wanaona aibu kurudi tena kwenye maisha yao ya wokovu, hii ni kwa sababu ya kutojihadhari na mambo mabaya. Hii ni kwa sababu hawakujihadhari na watu wanaotenda mambo mabaya.
Kuchukulia kawaida wale marafiki zetu wanaotenda mambo mabaya, imetugharimu sana tulio wengi, sababu hasa ya kutugharimu ni ile kuchukulia mambo kawaida. Bila kujua usipokuwa na tahadhari utajikuta umeingia kwenye tabia ile ile ya wale wanaotenda mambo mabaya.
Tembea na hili kwenye moyo wako, ili usije ukajisahau na kujiona upo salama sana, Kweli kuwa ndani ya Yesu upo sehemu salama kabisa ila sio kigezo cha kujiachia hovyo bila kuwa na tahadhari. Lazima uwe na tahadhari siku zote za maisha yako.
Hakikisha Neno la Mungu lipo kwa wingi moyoni mwako, litakusaidia sana kuepuka mitego mingi ya shetani, maana kuwa na tahadhari bila Neno la Mungu napo sio nzuri sana. Hakikisha unasoma Biblia yako kila siku, na kama unapenda tuwe pamoja katika hili tuwasiliane kwa wasap namba +255759808081.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com