
Tupo kwenye agano bora sana kuliko maagano yote yaliyopita huko nyuma, agano ambalo unaweza kufahamu mambo ya ndani zaidi. Ambayo huko nyuma hawakuweza kuyafahamu hayo mambo yaliyofichwa na Mungu.
Kitendo cha kumkiri Yesu Kristo kama Bwana na mwokozi wa maisha yako, kinakufanya uingie kwenye eneo ambalo litakufanya uwe na uwezo wa kuzijua siri za ndani za Mungu.
Mungu anaweza kukufunulia Neno lake kwa namna ambayo kwa akili za kibinadamu isingetegemewa/isingedhaniwa kabisa, lakini kwa kuwa wewe ni Mtoto wa Mungu. Unapata kuzijua siri za ndani ambazo Mungu anakufunulia mtoto wake kwa ajili ya kazi ile aliyokuandaa uifanye.
Tofauti kabisa na mtu ambaye hajaokoka, anaweza asikuelewe kabisa kutokana na mambo ambayo unafanya, na wale waliokoka wanaweza wakawa wanashangaa tu vile Mungu anakutumia kwenye eneo la utumishi alilokupa.
Watu wanaweza wakawa wanasoma Biblia zao kila siku, lakini kupitia maandiko yale yale waliyokuwa wanasoma kila siku, ukawafanya wawe na mshangao mkubwa baada ya kuhubiri au kufundisha kwa namna ya pekee kupitia andiko lile lile wanalolifahamu.
Hata vile unavyotazama mambo, ni tofauti kabisa na mtu ambaye hajaokoka, unaweza kuziona fursa za kuupata utajiri ule wa mbinguni. Maana aliye ndani yako ni mkuu sana, tena ndiye awezaye kufanya mambo makuu kupita akili za kibinadamu.
Ukiwa umempokea Yesu Kristo moyoni mwako sawasawa, vile unavyozidi kujaza maarifa mengi kwa kusoma Biblia yako, ndivyo unavyozidi kuzijua siri nyingi za Mungu. Mambo ambayo Mungu amekuandalia mtoto wake uliyempokea kama Bwana na mwokozi wa maisha yako.
Rejea: Siri ile iliyofichwa tangu zamani zote na tangu vizazi vyote, bali sasa imefunuliwa kwa watakatifu wake; ambao Mungu alipenda kuwajulisha jinsi ulivyo utajiri wa utukufu wa siri hii katika Mataifa, nao ni Kristo ndani yenu, tumaini la utukufu. KOL. 1:26-27 SUV.
Haleluya, kama nilivyoanza mwanzo kusema, agano jipya tulilonalo sasa hivi ni bora kuliko agano la kale, maana agano la kale halikuwa kama hili jipya la sasa. Agano la sasa watakatifu wote waliokaa vizuri na Yesu Kristo, wanao nafasi ya kufichuliwa siri ile Iliyofichwa zamani.
Kwanini usijivunie kuzaliwa mara ya pili? Kwanini usifurahie maisha ya ndani ya Kristo? Hakuna sababu ya kutofurahia maisha yako ndani ya Yesu Kristo. Maana unayo fursa nzuri sana ambayo haikuwepo hapo zamani ila sasa ipo kwa watakatifu wote.
Usikubali maisha yako ndani ya Yesu, usiwe msomaji wa Neno la Mungu, hakikisha unasoma Biblia yako kila siku, kupitia kusoma kwako maandiko matakatifu utajikuta unapokea mambo makubwa ya kuyafanyia kazi katika huduma uliyopewa na Mungu.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com
+255759808081