
Katika maeneo ambayo unapaswa kuyatilia uzito na kuyajengea umakini mkubwa sana katika maisha yako yako ya wokovu, ni eneo lako la kiroho. Uhusiano wako na Yesu Kristo unapaswa kuwa vizuri sana, kama utakuwa umeokoka lakini.
Jambo lingine la muhimu sana kama hujaokoka, utakuwa unakosa vitu vya muhimu sana katika maisha yako. Unaweza ukawa huoni sana kwa macho ya nyama ila kuna maeneo ambayo huwezi kufanya mambo makubwa kutokana na uhusiano wako mbaya na Mungu.
Sasa tukiacha yule ambaye hajaokoka, tuje kwa mtu aliyeokoka, ili aweze kufaidi matunda ya kuokoka kwake, anapaswa kufahamu/kujua nafasi yake mbele za Mungu. Anapaswa kujua yeye ni nani mbele za Mungu, akishajua Mungu ni Baba yake, na yeye ni mtoto wake.
Anaweza kufanya mambo makubwa akiwa anajua Mungu ni Baba yake, anaweza akawa na ujasiri mkubwa wa kufanya vitu bila hofu yeyote. Mtu wa namna hii itakuwa ni vigumu sana kumtisha na mambo yaliyo kinyume na mapenzi ya Mungu.
Zaidi mtu huyu akiwa ameokoka sawasawa, alafu akawa analijua Neno la Mungu na kuliishi kwa matendo, anaweza kupata faida nyingi sana za kuokoka kwake akiwa hapa hapa duniani.
Yesu akiwa ndani ya mtu, na mtu huyo akawa anajua aliyembeba ni nani, mtu huyo atakuwa ni wa viwango vingine kabisa, maana yapo mambo makubwa yatafichuliwa kwake.
Tena jambo lingine kubwa zaidi atakuwa amembaba Yesu ambaye ndani yake hazina zote za hekima na maarifa zipo kwake. Kujua hilo inamfanya mtu aliyeokoka aweze kufaidika na hayo yote ndani ya Yesu.
Rejea: Ambaye ndani yake yeye hazina zote za hekima na maarifa zimesitirika. KOL. 2:3 SUV.
Changamoto inakuja pale ambapo tunakuwa hatuna muda wa kusoma Neno la Mungu, au hatuna muda wa kusoma Biblia zetu. Jambo ambalo linatufanya tushindwe kujua mambo kama haya, na usipojua umembeba nani ndani yako, huwezi kuwa kama yule ambaye anajua amembeba nani ndani yake.
Kupitia usomaji wa Neno la Mungu, ndio mkristo anaweza kuzijua siri za Mungu juu ya maisha yake, ndio mkristo anaweza kumjua Yesu vizuri. Ndio kipindi ambacho hekima yake inazidi kuongezeka zaidi.
Tena Neno la Mungu linaongeza kiwango cha ufahamu wa maarifa ndani yake, inakuwa ngumu kwa mtu huyo Shetani kumlaghai au kumdanganya. Anaposhindwa kumdanganya maisha yake yanakuwa salama mbele za Mungu.
Tena unakuwa unajua ahadi za Mungu juu ya maisha yako kama mtoto wake, na kawaida unapojua Baba yako aliye juu mbinguni amekuahidi nini unakuwa na ujasiri wa kumdai pale utakapozikosa kuziona hizo baraka zako.
Rejea: Nami nitakupa hazina za gizani, na mali zilizofichwa za mahali pa siri, upate kujua ya kuwa mimi ni Bwana, nikuitaye kwa jina lako, naam, Mungu wa Israeli. ISA. 45:3 SUV.
Mungu mwenyewe anasema kupitia Neno lake, unayo ahadi mbele za Mungu, kitendo cha kumpokea Yesu kama Bwana na mwokozi wa maisha yako. Hizi ahadi ni zako, hazina zako zote zilizofichwa mahali ambapo kwa macho ya kawaida huwezi kuziona, Mungu anakufichulia.
Mjue sana Mungu ule mema ya nchi, utamjuaje sasa? Utamjua kadri unavyozidi kusoma Neno lake na kutafakari yale uliyosoma au uliyojifunza.
Hakikisha Biblia yako inakuwa rafiki yako wa kila siku, isome kila siku, na kama unataka kuungana na wenzako wanaosoma Biblia, tuwasiliane kwa wasap namba +255759808081.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com