Mtu kufanya jambo alafu wengine wakawa hawajali sana kile alichofanya au anachofanya, watu wengi huvunjika moyo na kuanza kufanya vitu kwa kiwango cha chini. Kule kufanya kwa bidii kunakuwa hakupo tena, kwa sababu alifanya vizuri alafu watu wakawa hawajamjali sana.

Wapo watu wengine wakikabidhiwa kazi fulani au jukumu fulani walifanye, watalifanya kwa kiwango cha chini sana, wanakuwa kama hawajali sana kile ambacho walipewa wafanye na walikubali kufanya hicho kitu.

Kutojali kile ambacho mtu alipewa afanye, kumewafanya wengi waonekane watu wa kawaida sana, ule uwezo wao ambao walipaswa kuonyesha kwenye kazi waliyokabidhiwa waifanye unakuwa mdogo sana. Na kusababisha ubora wa kitu walichopewa wakifanye kuonekana mdogo sana.

Shida ya kufanya vitu kwa kiwango cha chini, hakujawahi kumpa mtu sifa nzuri/njema, pamoja na hili bado watu wengi wanapuuza sana kufanya vitu kwa ubora kwenye nafasi zao walizopewa/walizonazo.

Wapo watu wamepata nafasi za uongozi katika maeneo mbalimbali, yaani katika maeneo ya kiroho na kijamii, anaweza akawa kiongozi wa kanisa au anaweza akawa kiongozi wa shule/chuo, anaweza akawa kiongozi wa mtaa/kijiji/kata/wilaya/mkoa nk.

Mtu huyo akashindwa kuitumikia vizuri nafasi yake aliyochaguliwa au aliyowekwa au aliyopewa, maana ndani yake hana msukumo wowote wa kuifanya kazi hiyo kwa moyo wake wote. Anachofanya yeye ni ilimradi siku ziende tu.

Hili linaingia hadi kwenye utumishi wa Mungu, kama ni mwimbaji wa nyimbo za injili, unamwimbia Mungu kwa moyo wako wote? Ukijua taji la kazi yako utalipokea kwa Bwana mwenyewe.

Ukiwa kama mtumishi wa Mungu kwa nafasi yako ya ualimu, nabii, mtume, mwinjilisti, na mchungaji, unamtumikia Mungu kwa moyo wako wote? Bila kujalisha wangapi wanakutia moyo, au unafanya kazi ya Bwana kiulegevu?

Rejea: Lo lote mfanyalo, lifanyeni kwa moyo, kama kwa Bwana, wala si kwa wanadamu, mkijua ya kuwa mtapokea kwa Bwana ujira wa urithi. Mnamtumikia Bwana Kristo. KOL. 3:23‭-‬24 SUV.

Ndugu yangu, kazi yeyote utakayopewa na ukaikubali kuifanya kazi hiyo, hakikisha unaifanya kwa moyo wako wote ukijua unafanya kwa Bwana, usikubali kupewa majukumu ambayo watu wanaamini utafanya vizuri. Alafu ukaja kufanya kwa mkono mlegevu, hilo halitakiwi kabisa.

Mtumishi wa Mungu, mtumikie Mungu wako kwa moyo wako wote, usiangalie watu, kuna wakati hutaonekana sana kama unafanya jambo la maana. Hilo lisikuvunje moyo, endelea kufanya huduma uliyopewa kwa moyo wako wote ukijua unafanya kwa Bwana.

Umeamua kusoma Biblia yako kila siku, usifikiri kila siku utaamka unajisikia kusoma hiyo Biblia yako, zipo siku utajikuta hujisikii kabisa. Kama ulikuwa husomi kwa moyo, utaishia njiani, hasa pale utakapokutana na changamoto ngumu za maisha.

Chochote utakachoamua kufanya au utakachoambiwa fanya, hakikisha unalifanya kwa moyo wako wa upendo, usilifanye huku moyo wako umesinyaa. Kufanya huku moyo huna furaha nalo, hilo jambo halitakuwa na matunda mazuri.

Hili linaingia kwenye maeneo yote ya maisha yako, yaani ya kiroho na kimwili, chochote kile ilimradi hakimkosei Mungu, hakikisha unakifanya kwa moyo. Usifanye jambo/kitu ilimradi unafanya, ukishafikia hatua ya kufanya ilimradi unafanya ujue hilo jambo halikufai tena.

Kama bado hujajiunga na kundi letu la wasap la kusoma Neno la Mungu kila siku, nichukue nafasi hii kukukaribisha, tuma ujumbe wako kwa wasap namba +255759808081 utaunganishwa kwenye kundi hili.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com