Muda tulionao ni mchache sana, japo kuna watu huwa tunaona tuna muda wa kutosha ila ukilitafakari vizuri hili utaona jinsi gani muda tulionao nao ni mchache sana.

Mambo ni mengi sana ya kufanya ila kutokana na muda, huwezi kuyafanya yote kwa pamoja, lazima uchague mambo machache ya kufanyia kazi. Bila kufanya hivyo unaweza kujikuta unagusa gusa kila kitu, na mwisho wake unajikuta hakuna ulichokifanya.

Utakuja kuona hakuna ulichokifanya cha maana sana, hii ni baada ya kutathimini kila jambo ulilokuwa unalifanya, utaona hakuna matunda yeyote uliyozalisha. Zaidi sana umepoteza muda wako mwingi kwa kugusa gusa kila jambo, bila kuwekea umakini hadi uhakikishe kitu kimeleta matokeo.

Kuukomboa wakati kwa kila mmoja wetu ni jambo la kuzingatia sana, wala sio jambo la kupuuza hata kidogo, japo wengine tunaweza kuona tunao muda wa kutosha sana.

Wewe ukiwa mtumishi wa Mungu, hupaswi kuutumia muda vibaya, muda ulionao unapaswa kuuona kama lulu, hata unapokuwa umekaa mahali popote pale unapaswa kujihoji kila wakati kuna kitu unaingiza. Ili ukitoka hapo uwe umeongeza kitu cha kukusaidia katika huduma uliyopewa na Mungu, au uwe umeacha alama nzuri.

Hata kwa wale wasioamini hatupaswi kutumia muda mwingi sana kwao, sio kuanzia asubuhi hadi jioni upo naye tu unamwambia habari za kumwamini Yesu Kristo. Badala yake utakuwa kero kwake na lile ulilomweleza linaweza lisiingie sana kwake.

Tusishinde muda mrefu kwa wasioamini, yaani usikae kwa mtu mmoja muda mrefu kumshuhudia habari za Yesu Kristo, kaa naye muda ule ambao utamweleza yale uliyotakiwa kumwambia kisha mwachie nafasi ya kufanya maamzi.

Muda ni mchache, unapaswa kupeleka injili na mahali pengine, kukaa na mtu mmoja kutwa nzima ni kupoteza muda ambao unapaswa kumpelekea mwingine habari za Yesu. Hapa washuhudia wa nyumba kwa nyumba tunapaswa kuzingatia sana hili.

Unaweza kukutana na mtu ambaye hajaokoka, ukasumbuana naye kwa maswali weee, bila kuangalia muda wako, utashangaa unamaliza masaa mengi na asikuelewe chochote.

Rejea: Enendeni kwa hekima mbele yao walio nje, mkiukomboa wakati. KOL. 4:5 SUV.

Tumia hekima, kuna maeneo ambayo utafika utapaswa hekima iliyo ndani yako itumike, bila kutumia hekima badala ya kuwa baraka utakuwa kero isiyozaa matunda mema. Japo unaweza kufikiri unafanya kazi ya Bwana, lakini kuna eneo unakosa hekima.

Maandiko yanatuasa tuukomboe wakati, na tuukomboe kweli wakati, bila kufanya hivyo utajikuta umri wetu umeenda bila kuzalisha matunda ya kutosha. Ambapo tungetumia wakati wetu vizuri tungeweza kuzalisha matunda mengi zaidi.

Mfano rahisi ni huu, utakuta mama/dada anaamka asubuhi anaenda kwa rafiki yake au kwa mama/dada mwenzake kushinda naye kutwa nzima. Huyu mama/dada anapoteza muda wake, unakuta wanachokizungumza hakina hata utukufu kwa Mungu.

Komboa wakati ndugu unayesoma ujumbe huu, usikubali muda wako utumike vibaya, wala usikubali kupoteza muda wako mahali popote. Muda wetu ni mchache sana, tuutumie vizuri kwa mambo ya msingi.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com