Zipo tabu nyingi sana tunazipitia au tunakutana nazo kwenye maisha yetu, tabu hizi au dhiki hizi wakati mwingine zinatufanya tuonekane kama vile hatuna Mungu aliye hai.

Mungu tunaye, bila kujalisha mazingira magumu tunayopitia, wala hupaswi kuumizwa na mtu yeyote yule, hasa pale unapokuwa kwenye tabu ngumu kwenye maisha yako. Amini Mungu yupo pamoja nawe.

Kuokoka kwetu hakutufanyi tusipatwe na dhiki za dunia hii, pamoja na uhusiano wetu na Mungu upo vizuri, bado tutaandamwa na mambo mbalimbali magumu ya kutuumiza mioyo yetu.

Huenda ulishaanza kujiona uhusiano wako na Mungu haupo vizuri kutokana na shida au tabu unazopitia, hayo mawazo sio sahihi kabisa, kama unajua hujamtenda Mungu dhambi na dhamiri yako inakushuhudia hivyo. Huna haja kuwaza kuhusu uhusiano wako na Mungu labda haupo vizuri.

Dhiki yako isikufadhaishe kiasi kwamba ukakosa furaha ya maisha yako, furaha yako iendelee kudumu ndani ya Yesu Kristo. Bila kujalisha upo kwenye hali gani, bila kuangalia unaandamwa na matatizo gani.

Rejea: Mtu asifadhaishwe na dhiki hizi; maana ninyi wenyewe mnajua ya kuwa twawekewa hizo. 1 THE. 3:3 SUV.

Iwe unapitia dhiki kwenye utumishi wako hilo lisikuondoe kwenye huduma uliyopewa na Mungu, iwe unapitia dhiki kwenye ndoa yako tumaini lako lisiondoke kwa Bwana.

Iwe wazazi wako wanapita kwenye dhiki au tabu mbalimbali, imani yako kwa Yesu Kristo isitetereke kamwe. Endelea kusimamia wokovu wako, endelea kusonga mbele pasipo hofu yeyote.

Mwisho wa siku hayo yatapita na utaendelea kumwona Yesu kwa kiwango cha juu zaidi, na hutobaki kama ulivyo, tena utakuwa shuhuda mzuri kwa wale wasiokoka. Kupitia mambo magumu uliyokuwa unapitia uliendelea kumtumainia Bwana Yesu, utawafanya wajue unaye Mungu wa kweli.

Mwisho, nakusihi sana usije ukaacha kusoma Neno la Mungu kwa sababu ya dhiki unazopitia katika maisha yako, kitendo cha kuacha kusoma Neno la Mungu kwa kigezo cha kupitia mambo magumu. Kutakufanya ushuke zaidi kwa kuruhusu udhaifu.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com