Kujiweka vizuri kwenye maisha yako ya wokovu, kuwa siriazi na mambo ya Mungu, sio tu ni jambo linalokuletea faida mwenyewe. Kuishi maisha ya kumpendeza Mungu wako ni jambo linalowafanya watu wengine wajivunie kuhusu wewe.

Wapo wazazi wa kiroho na kimwili wanakuwa wanajivunia kuhusu mtoto wao mwenye tabia nzuri, wapo walimu wanakuwa wanajivunia kuhusu mwanafunzi wao mwenye tabia nzuri na mwenye mafanikio mazuri.

Wapo marafiki zako uliosoma nao wanakuwa wanajivunia kuhusu wewe, hata wanapokuwa mahali fulani wanasema fulani tumesoma naye yule. Haiji hivi hivi inakuja pale unapokuwa unafanya mambo mazuri yakuwafanya watu wengine walazimike kuiga mfano mzuri kutoka kwako.

Wengi wetu huwa tunaona tukiwa na mienendo safi ya kumpendeza Mungu, huwa tunafikiri ni kwa faida yetu tu, hapana, zipo faida nyingi sana za kuwasaidia na wengine ambao bado hawajamjua Yesu.

Kuishi kwako/kwangu maisha ya kumpendeza Mungu, kunawafanya viongozi wetu wanaotuongoza wajivunie kuhusu sisi, hata wanapokuwa mahali fulani wanakuwa wanajivunia kuhusu sisi. Na kweli wanakuwa wanasema kile ambacho ni cha kweli.

Kuishi kwako maisha ya kumpendeza Mungu ni fahari kubwa sana kwa mchungaji wako, ama kwa mzazi wako aliyekuzaa, ama kwa yule mtumishi aliyekuhubiria injili ukaokoka.

Wanapokuangalia maendeleo yako, wanakuwa wanajisikia fahari kubwa sana, fahari ambayo inawafanya waendelee kumtukuza Mungu kwa ajili yako. Wakati mwingine huenda usijue hilo au unaweza kuchelewa kujua hilo ila kupitia ujumbe huu unapaswa kujua.

Rejea: Hata na sisi wenyewe twaona fahari juu yenu katika makanisa ya Mungu kwa ajili ya saburi yenu, na imani mliyo nayo katika adha zenu zote na dhiki mnazostahimili. 2 THE. 1:4 SUV.

Kupitia andiko hili linatuthibitishia kuhusu hili ninalokuambia hapa, kusimama kwetu na Yesu Kristo sawasawa wapo watu wanafurahia mno kusimama kwetu vizuri. Ni kama jambo lisilowahusu sana ila kutulia kwako kwa Yesu Kristo ni fahari kubwa sana kwa wengine.

Unapojitahidi kutunza maisha yako ya wokovu, lipo kundi linalofurahia sana, lipo kundi linalojivunia kupitia wewe, kuna watu wakitaka kutoa mifano kwenye mazungumzo yao. Lazima wakutolea mfano mzuri wewe, unaweza usijue ila huo ndio ukweli.

Kumpokea kwako Yesu Kristo na kuendelea kuishi maisha yanayompendeza yeye, sio tu utaenda mbinguni, Mungu mwenyewe anajivunia kuhusu wewe. Na wapo watu wanaoona fahari kubwa kuhusu wewe, achana na wale ambao wanakupiga vita, lipo kundi lingine linaloona fahari kupitia wewe.

Hasa watumishi wa Mungu wanaohubiri injili, wanapokuona umeokoka alafu ukawa unaendelea vizuri, na unaonyesha bidii ya kuendelea kukua zaidi kiroho. Kwa mtumishi wa Mungu wa kweli, lazima aone fahari juu yako.

Kwahiyo fahamu kuokoka kwako na kutunza maisha yako ya wokovu, ni fahari kubwa sana kwa watu wengine, wanaweza wasikuambie moja kwa moja ila unapaswa kufahamu hili kwa mjibu wa maandiko.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com
+255759808081