
Matatizo mengi yanayowapata watu ni pale wanapoipuuza kweli ya Mungu au ni pale wanapoikataa kweli ya Mungu, kuikataa kweli ya Mungu imewafanya watu wengi kuingia kwenye mashimo ambayo wapo ambao wameshindwa kutoka humo hadi leo.
Japo ukweli muda mwingine huwa unaonekana ni mchungu sana, japo ukweli huwa unaonekana kama ni mgumu sana kuufuata, huwa unaokoa mambo mengi sana. Tena huwa unadumu siku zote, tofauti kabisa na mtu ambaye aliamua kupita njia rahisi ya uongo.
Uongo unaweza kuonekana ni mrahisi kufuata ila shida yake huwa haumfikishi mtu kwenye hatima yake, hata kama ataonekana kustawi sana. Mwisho wake huwa mbaya sana, ambapo mwisho ndio unaangaliwa sana na Mungu kuliko hata mwanzo.
Sasa mtu anapoukataa ukweli, mtu huyo ni ngumu sana kuokolewa na Yesu Kristo, maana wapo watu wamefungwa kwenye mapokeo potovu na wakihubiriwa injili ya kweli ya Kristo wanaona yale ya kwao wanayoyaamini ndio sahihi zaidi.
Watu kama hao mwisho wao huwa ni jehanamu wasipobadilika, wakati walikuwa na uwezo wa kuepuka kutupwa jehanamu. Na wakati walikuwa na nafasi ya kutengeneza na Mungu wao, bila kujalisha walikuwa kwenye uongo muda mrefu.
Jambo lingine ambalo litaendelea kuwatesa hapa duniani watu wasiopenda kweli ya Mungu, wataendelea kudanganywa zaidi ili kuendelea kuimarika katika uongo huo.
Hili tunajifunza kupitia maandiko, sio maneno ya kuokota barabarani, tunasoma kupitia Biblia, inaonyesha wanaopotea kwa mafundisho potovu ni wale ambao hawakuipenda kweli ya Mungu.
Rejea: Na katika madanganyo yote ya udhalimu kwa hao wanaopotea; kwa sababu hawakukubali kuipenda ile kweli, wapate kuokolewa. 2 THE. 2:10 SUV.
Kumbe wanaopotea sio kana kwamba hawakusikia kweli ya Mungu, wapo wanaopotea kwa sababu hawakukubali kuipenda kweli ya Mungu. Kwa maneno mengine tunaweza kusema walisikia vizuri injili ya Yesu ila wameikataa kuikubali.
Ina maana kwamba wapo watu wataingia jehanamu ya milele sio kwa sababu hawakuisikia kweli ya Mungu, watakuwa waliisikia kabisa ila hawakukubali hiyo kweli waliyoambiwa au waliyofundishwa au waliyohubiriwa nayo.
Mungu akupe neema ya kusoma hili somo kwa sura ambayo itakupa picha halisi ili uweze kulielewa kwa undani zaidi, maana unaweza kulichukulia hili suala kwa kawaida alafu baadaye likakuletea shida.
Haijalishi mafundisho potovu yamekuwa mengi sana, fahamu kwamba bado yapo mafundisho sahihi ya Neno la Mungu, hasa ukiwa msomaji wa Biblia yako. Utaweza kuthibitisha hili kupitia kwa watumishi wa Mungu wanaohubiri kweli yake.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com