Moja ya vitu vya kupiga vita katika maisha yako ni uvivu, hakuna jambo baya kama uvivu, hakuna mtu anayetaabika kwenye maisha yake kama mvivu. Uvivu huzaa kitu kuchagua kazi, uvivu huzaa sababu nyingi za kushindwa.

Uvivu ndani ya mtu ni kumfanya asifanye kile ambacho kina manufaa kwenye kesho yake, uvivu huzaa mtu awe na maneno mengi sana ya uongo. Mtu mvivu hana tofauti sana na mtu tapeli, na ukichuguza sana utakuta hadi mtu kuwa tapeli chanzo chake kimeanzia kwenye uvivu.

Shida kubwa ambayo ipo kwa watu wavivu, watu wasiopenda kazi huwa wanapenda sana kujishughulisha na mambo ya watu, utakuta kuanzia asubuhi hadi jua linazama. Kazi yake huyu mtu anakuwa anafutilia maisha ya watu wengine.

Siku hizi linatumika neno “UMBEA” watu wengi wambea kupitiliza, asilimia kubwa ni wavivu, kama sio mvivu basi atakuwa anakusanyiwa habari na mvivu. Kisha anamtumia mvivu yule yule kusambaza kile ambacho amemwambia, alafu yeye anaendelea na shughuli zake.

Kuna kauli moja imekuwa kama msemo wa watu, japo sijui kama inafanyiwa kazi, na sina uhakika sana kama wote wanaotumia kauli hiyo kama wanajua kuwa ni andiko ndiyo linasema hivyo.

Kauli yenyewe ni “ASIYEFANYA KAZI NA ASILE” bila shaka sio jambo geni kwako, kwa namna moja ama nyingine utakuwa umewahi kusikia hii kauli watu wakiisema.

Pamoja na watu kusema sana hii kauli, nikuambie kuwa ni kauli ambayo imenukuliwa kwenye andiko takatifu, nitaenda kukuonyesha hapa ili uweze kuelewa sio misemo ya watu waliyojitungia wenyewe.

Rejea: Kwa kuwa hata wakati ule tulipokuwapo kwenu tuliwaagiza neno hili, kwamba IKIWA MTU HATAKI KUFANYA KAZI, BASI, ASILE CHAKULA. 2 THE. 3:10 SUV.

Umeona hapo, hili ni agizo ambalo lipo kimaandiko kabisa, wale wasiofanya kazi wasile chakula, utakubaliana nami mtu asipolima wakati wa masika/mvua. Na mtu huyo anategemea kilimo ndio ale chakula, uwe na uhakika hali ya mtu huyo itakuwa mbaya.

Sasa wale watu wavivu, watu wasioenda kwa utaratibu, hawana mikakati ya kufanya kazi, wao wakiamka ni kujishughulisha na mambo ya wengine. Fulani yupo hivi, fulani yupo vile, fulani kafanya hivi, fulani kafanya vile, hadi jua linachoea yeye anahangaika na mambo ya wengine.

Muda wa kuhangaika na mambo ya wengine anao ila muda wa kuhangaikia mambo yake hana, unaweza kuta hata kitu cha kula hana au hajui ila anakesha kuseng’enya watu. Sasa hili nalo biblia imelisemea;

Rejea: Maana twasikia kwamba wako watu kwenu waendao bila utaratibu, hawana shughuli zao wenyewe, lakini wanajishughulisha na mambo ya wengine. 2 THE. 3:11 SUV.

Watu wa tabia hii mtume Paulo aliwabaini, ambapo hata leo sio kana kwamba hawapo, wapo kabisa na tunao katika mazingira tunayoishi, kama sio wewe basi ni ndugu yako, na kama sio ndugu yako basi ni rafiki yako, na kama sio rafiki yako ni jirani yako au mshirika mwenzako.

Wewe mwenye tabia hii unaonywa, uachane kabisa na kazi hiyo, jikite kwenye shughuli zako, achana na kukesha ukijishulisha na mambo ya watu. Tena mambo yenyewe hayana hata taji mbinguni zaidi unajikosesha kwa Mungu.

Rejea: Basi twawaagiza hao, na kuwaonya katika Bwana Yesu Kristo, watende kazi kwa utulivu na kula chakula chao wenyewe. 2 THE. 3:12 SUV.

Fanya kazi kwa bidii acha majungu, amka mapema ukafanye kazi kwa bidii acha kulala mpaka saa mbili, acha kusubiri watu wakuletee amka na wewe ukatafute, tafuta na wewe cha kwako na familia yako.

Hata kama kazi inaonekana ni ya kipuuzi kwa wengine, maadam haimkosei Mungu wako, inuka kafanye kazi, kama unafanya tayari usikubali kuyumbishwa na mtu yeyote. Maana hiyo ndio kazi yako inayokufanya ulishe familia yako, hiyo ndio inayokufanya usomeshe watoto wako.

Kama una tabia ya kuomba sana fedha kwa watu nakuagiza uache hiyo tabia badala yake omba mtaji ufanyie kazi uzalishe na wewe, ukianza kuzalisha hutoomba tena. Bali na wewe utageuka msaada kwa wengine ambao na wao bado hawajafikia hatua kama yako.

Achana kabisa na mambo ya watu, sijui fulani kafanya hivi na vile, hayakuhusu, uvivu huo ulionao unaulea mwenyewe na usipoukataa utakufanya uwe masikini kila eneo la maisha yako. Huwezi kufanikiwa kwenye huduma kama ni mvivu.

Huwezi kuwa mwalimu mzuri wa Neno la Mungu kama ni mvivu wa kujifunza, utaishia kuwa kawaida tu ambapo halikuwa kusudi la Mungu uishie kuwa kawaida. Mungu anakuta ufikie viwango vya juu zaidi kwa ajili ya utukufu wake, pale utakapoitenda kazi yake kwa viwango, utukufu unamrudia yeye.

Haya tunayapata kwa sababu tunasoma biblia zetu, hata kama ulikuwa na katabia fulani kasikoendana na mtu aliyeokoka sawasawa. Basi kupitia kujifunza kwake anakutana na haya ili aweze kubadilika eneo ambalo lilikuwa lina shida.

Hakikisha unasoma Biblia yako ya Neno la Mungu kila siku, katika kusoma kwako mwambie Roho Mtakatifu akufunulie uweze kuelewa sawasawa na ilivyokusudiwa uelewe. Usisome tu Neno la Mungu juu juu ilimradi umesoma, soma kwa kumaanisha haswa, utaona mabadiliko ndani yako.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com