Kila mmoja anaweza akawa mtumishi wa Mungu ikiwa tu ameokoka, anaweza kumtumikia Mungu kwa kuwaeleza wengine habari za Yesu Kristo. Na hao atakaowahubiria habari za Yesu, wakaamua kumpokea Yesu kama Bwana na mwokozi wao.

Mwingine anaweza akawa mtumishi wa Mungu katika nafasi yake ya kazi anayofanyia, huyu naye anaweza akawa anamzalia Mungu matunda kwa namna ambayo anakuwa anawajibika kwenye nafasi aliyonayo.

Yupo mtu mwingine anakuwa anafanya kazi ya kitumishi ya kuchunga kundi la watu, anakuwa analiekeza njia sahihi ya kuishi maisha yanayompendeza Mungu wao. Na kuwaonya pale wanapoenda kinyume na mapenzi ya Mungu, na kuwafundisha yale yawapasayo kutenda.

Kila mmoja anaweza kujiita mtumishi wa Mungu lakini asifiwe na sifa ya mtumishi, ili mtu awe mtumishi wa Mungu, zipo sifa ambazo zitamtambulisha huyo mtu kuwa yeye ni mtumishi wa kweli wa Mungu.

Na hadi mtu aitwe mtumishi wa Mungu kipo kigezo ambacho kimemfanya huyo mtu kuchaguliwa katika nafasi yake ya utumishi, hili linaweza kutumiwa na mtumishi yeyote kumrithisha mtoto wake wa kiroho huduma aliyokuwa anaifanya.

Sifa hiyo ni “UAMINIFU” hii ndio sifa kuu ambayo inaweza kumfanya mtu akachaguliwa kuchunga kanisa, hii ndio sifa ambayo inaweza kumfanya mtu akachaguliwa na Mungu katika kuhubiri injili ya Kristo. Na mtu huyo Mungu akamtumia kama chombo chake kwenye utumishi wake.

Rejea: Nami namshukuru Kristo Yesu Bwana wetu, aliyenitia nguvu kwa sababu aliniona kuwa mwaminifu, akaniweka katika utumishi wake. 1 TIM. 1:12 SUV.

Hichi ndicho kilichomfanya Paul akawekwa na Mungu katika nafasi yake ya utumishi, unaweza kuona jinsi gani uaminifu ulivyo wa muhimu sana kwa mtu yeyote aliyempokea Kristo moyoni mwake.

Uaminifu unaweza kutumika kwenye maeneo mengi sana ya maisha ila mtu akiwa mwaminifu mbele za Mungu, Mungu anaweza kumpa jukumu la kumtumikia kwa namna ambayo Mungu atataka atumike.

Hili linaweza likawa msaada kwa wale ambao wanapenda sana kutumikia Mungu, na wanatamani Mungu awatumie kwenye utumishi wao ila uaminifu kwao unakuwa haupo kabisa. Kama tulivyoona kitu kilichomfanya Paul awekwe kwenye nafasi ya utumishi ilikuwa ni uaminifu wake.

Jambo lingine ambalo tunaliona kwenye mstari huu ni “KUTIWA NGUVU” mtume Paulo alitiwa nguvu na Mungu kwa sababu alimwona kuwa mwaminifu. Hili ni la kuzingatia sana, kumbe uaminifu wetu unaweza kutumika kwa Mungu kutupatia nguvu zake.

Hebu jaribu kujiuliza, Je! Uaminifu wako mbele za Mungu upo vipi? Kama haupo vizuri ni vyema ukachukua hatua kuanzia sasa. Maana uaminifu wako mbele za Mungu ni wa muhimu sana.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com