Moja ya vitu vya kuzingatia ni pamoja na hili la ushemasi, japo linaweza kuonekana ni jambo la kawaida au anaweza kuonekana ni mtu asiye wa muhimu sana ndani ya kanisa. Lakini ni moja za huduma za muhimu sana kuwepo kanisani.

Shemasi anachaguliwa na mchungaji wake au na meza yake mchungaji, hadi mtu kufikia hatua ya kuwekewa mikono ya ushemasi, anapaswa awe amepitia vigezo/ngazi/michujo kadhaa.

Moja ya kigezo hicho anapaswa awe na tabia njema, asiwe na tabia yeyote chafu, tabia inayomfanya asomeke vibaya kwa jamii au wale majirani zake wanaomzunguka mtaani kwake.

Tena anapaswa kufanyiwa majaribio kadhaa kama kweli anauweza ushemasi anaotaka kupewa, anaweza kujaribiwa akiwa anajua au akiwa hajui kabisa. Akiwa hajui ndio nafikiri itapendeza zaidi maana hataigiza uzuri, wala hataficha uhalisia wake.

Rejea: Hawa pia na wajaribiwe kwanza; baadaye waitende kazi ya shemasi, wakiisha kuonekana kuwa hawana hatia. 1 TIM. 3:10 SUV.

Unaona hilo andiko linavyosema, sio maneno tu, ni maelekezo tunayopata kutoka ndani ya Biblia zetu, hapa mtume Paulo anampa maelekezo Timotheo. Maelekezo ambayo yanaweza kutumika kutusaidia kupata watu sahihi wa kusimama katika nafasi zao za ushemasi.

Unaweza ukamwona mtu ameokoka vizuri sana, ukimfuatilia kwa makini unaweza ukamkuta yupo tofauti kabisa na vile unamwona siku za ibada za pamoja. Ndio maana tunasoma kuwa wanapaswa kujaribiwa kwanza kabla ya kupewa nafasi za ushemasi.

Hili linaweza kuingia karibia maeneo yote hasa pale tunapotafuta kiongozi, au mtu wa kutusaidia kazi zetu, iwe nyumbani, au iwe kwenye biashara zetu, au iwe kwenye mahusiano.

Hayo ni mambo baadhi ya kuzingatia pale unapotaka/mpotaka kuchagua Shemasi, jambo lingine la kuzingatia sana ni mke wa Shemasi anapaswa kuangaliwa pia tabia zake.

Tumeona Shemasi anapaswa kuwaje, kama Shemasi ni mwanaume, mke wake anapaswa kuwa na tabia njema, asiyeseng’enya watu, mwenye kiasi, na mwaminifu katika mambo yote.

Rejea: Vivyo hivyo wake zao na wawe wastahivu; si wasingiziaji; watu wa kiasi, waaminifu katika mambo yote. 1 TIM. 3:11 SUV.

Itakuwa ajabu kama Shemasi ana mke asiye na tabia njema, mseng’enyaji, asiye na kiasi, na asiye mwaminifu katika mambo yote. Huyu mwanamke hapaswi kuwa mke wa Shemasi, kama ni mke wake tayari basi amekosa sifa.

Ndio maana tuliona mwanzo kuwa kabla ya mtu kuteuliwa kuwa Shemasi, anapaswa kufanyiwa uchunguzi wa kina, bila kufanya hivyo tutakuwa na mashemasi wasiokuwa na sifa.

Shemasi anaweza asionekane wa muhimu sana ila tunapaswa kuelewa kuwa ni chombo cha muhimu sana kanisani, wanaosoma Neno la Mungu hili haliwezi kuchukuliwa kama jambo la kawaida.

Kupitia ujumbe huu rudi kwenye msingi wa Neno la Mungu, kama tulikuwa tunachukulia mambo kawaida kawaida, kuanzia sasa tuache kufanya hivyo ili tuwe na mashemasi wazuri wanaolifaa kanisa la Bwana Yesu.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com