Leo ni siku ya maalumu kwa wakristo wote duniani wanaanzimisha siku ya kumbukumbu ya kufufuka kwa mwokozi wa ulimwengu, Yesu Kristo. Ni siku muhimu sana ya kujikumbusha kuwa wokovu tulionao, yupo aliyegharimia kwa gharama kubwa sana.

Wakati tunaendelea kuadhimisha siku ya kufufuka kwa mwokozi wetu Yesu Kristo, wapo watu wanafurahia siku hii kwa kukaa na familia zao huku wakifurahi pamoja kwa kula na kunywa. Na wengine wakiwa wanafurahia tu uzima walionao hadi sasa, japo hawana chakula kizuri sana cha kula.

Wapo pia siku kama ya leo imewakuta wakiwa hawana amani kabisa mioyoni mwao, sio kana kwamba hawakuwa na nguo mpya, sio kana kwamba hawakuwa na chakula kizuri, sio kana kwamba wamefiwa na ndugu zao. Ni vile tu yapo mambo ya zamani yanawaumiza mioyo yao.

Hili limekuwa janga la wengi sana, wapo watu afya zao zinazidi kuharibika kwa sababu ya mambo yaliyopita, hadi leo anajiuliza kwanini ilitokea kwake, hadi leo anajiuliza kwanini aliachwa na mchumba wake aliyempenda.

Hadi leo yupo mtu anaumia sana kwa kufukuzwa kazi, miaka mingi imepita ila kitendo cha kufukuzwa kazi bado kinamtesa ndani ya moyo wake, mwingine anateswa na hasara iliyotokea kwenye biashara yake miaka mingi iliyopita.

Yupo mwingine anateswa na mambo mabaya aliyowahi kutenda huko nyuma kabla hajaokoka, wakati mwingine akitaka kufanya kazi ya Mungu anashindwa kwa sababu ya zile kumbukumbu mbaya ndani yake zinazomjia.

Yupo mwingine anateswa na kufiwa na mume/mke wake, miaka mingi sana imepita lakini bado anateswa na kuondokewa na mpendwa wake. Hana amani, ana machozi mengi sana ya ndani kwa ndani, wakati mwingine anashindwa kujizuia na kuonyesha wazi hayo machozi.

Mwingine anateswa na hali ya kufiwa na baba/mama yake, miaka mingi imepita ila bado picha ya mzazi/wazazi wake bado haijafutika kichwani mwake. Kila wakati amekuwa mtu ambaye hana amani, hata ule uhodari wake umeshuka kwa kiwango cha juu sana katika shughuli zake.

Pamoja na hayo yote ya kuumiza mioyo yetu, tumeamriwa tusiyakumbuke mambo ya zamani au yaliyopita, wala tusiyatafakari hayo mambo ya zamani.

Rejea: Msiyakumbuke mambo ya kwanza, wala msiyatafakari mambo ya zamani. Isaya 43:18.

Ndugu yangu, anza mwanzo mpya, achana na mambo yaliyopita, mambo ambayo yanautesa moyo wako, usikubali kuendelea kuteswa na mambo ya zamani.

Kuendelea Kuyakumbuka hayo mambo yaliyopita na kuendelea kuyatafari sana, hakuna jambo utaweza kubadilisha zaidi ya kuendelea kujiumiza. Ulipo sasa ndio unaweza kufanya jambo la tofauti katika maisha yako na jina la Yesu Kristo likatukuzwa katika maisha yako.

Achana kabisa na mambo yaliyopita, ukiona ni ngumu kutoka, ingia kwenye maombi ya kufunga na kuomba, maana yapo mambo hayatoki hadi kwa kufunga na kuomba.

Rejea: [Lakini namna hii haitoki ila kwa kusali na kufunga.] Mathayo 17:21.

Pasaka hii iwe kumbukumbu kwako kuwa uliondokana na kuteswa na mambo yaliyopita, anza kuishi maisha yasiyo na maumivu ya mambo yaliyopita. Tua mzigo wa mambo yaliyopita, uwe huru moyoni mwako sasa katika jina la Yesu Kristo wanazareti.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com