
Wapo watu wamekuwa wakichukia sana hichi kitendo cha kukemewa/kuonywa hadharani, wamekuwa wakiona kama hawatendewi haki. Wengine wanaona kama wamekosea kwanini wasingeitwa pembeni au ofisini au nyumbani wakaonywa/wakakemewa.
Ukweli usiopingika ni kwamba kuonywa au kukemewa mbele za watu au mbele ya hadhara, inaleta fedheha kubwa sana kwa mtu, lakini kosa anakuwa ametenda kabisa. Tena kosa lenyewe alilotenda ni la aibu kabisa.
Wapo watu wameenda mbali zaidi na kuona sio jambo la kistarabu kuonywa/kukemewa hadharani mbele ya watu au mbele ya washirika, wanaona kiongozi wa kanisa anakuwa hajatumia busara.
Wengine huenda mbali zaidi na kufikiri ni kukosa hekima au maarifa kwa mchungaji au kiongozi anayewaongoza, wanaanza kufikiri angetumia njia nyingine ila sio hiyo ya kuwakanya hadharani. Tena wakati mwingine watoto wao au familia zao zinakuwa zinasikia au zinaona.
Kile ambacho wamekitenda wanakuwa hawakioni tena kama kina uzito sana, uzito unakuwa pale wanapokemewa hadharani, hapo ndipo wengine huhama na makanisa kwa sababu ya kukemewa hadharani.
Kwanini sasa watumishi au viongozi hukemea au huonya watu hadharani? Lipo jibu la hili swali, kufanya hivyo sio kana kwamba kiongozi anakuwa hajui kitu. Lipo kusudi lake la kufanya hivyo, yeye kama mchungaji au kiongozi wa kanisa, sio mara zote atawaonya/atawakemea ofisini kwake.
Wala sio wakati wote mchungaji atakemea dhambi tu kwa ujumla bila kuwataja wahusika, wakati mwingine atakemea dhambi mbele ya kanisa kwa kuwataja wahusika. Ili iweje sasa? Ili wengine watakapotazama au watapoona kile kitendo waweze kuogopa kutenda lile lile kosa au ile ile dhambi.
Rejea: Wale wadumuo kutenda dhambi uwakemee mbele ya wote, ili na wengine waogope. 1 TIM. 5:20 SUV.
Hilo ndilo kusudi haswa la viongozi wa kanisa kukemea dhambi hadharani kwa kuwataja wahusika, sio kana kwamba walikuwa hawawezi kuwakemea wakiwa peke yao. Wanafanya hivyo ili washirika wengine wasije wakaona haina shida kufanya dhambi aliyoifanya mwenzao.
Wasipofanya hivyo wapo washirika wataanza kuona kufanya dhambi fulani ni sahihi kabisa, hii ni kutokana na kumwona mwenzao akiwa amefanya dhambi fulani iliyojulikana na kila mmoja. Alafu mtu huyo akawa hajakemewa, wataona kumbe ni sahihi na wao kufanya.
Sio wote waliopo kanisani wanajua kujisimamia wenyewe, wapo bado wachanga kiroho, wanapoona jambo fulani baya limetendeka. Halafu mchungaji akawa hajalikemea hilo jambo ambalo mwenzao amelifanya, wataona ni zuri kufanya na wao.
Kwahiyo tusiwaone wachungaji au viongozi wanavyokemea dhambi hadharani na wanamtaja mhusika, tukawaona hawatendi haki. Tunapaswa kujua maandiko matakatifu yanasemaje kuhusu hili, tumeona wana kibali cha kufanya hivyo.
Wanaelewa sana wanachofanya, na yapo mambo ambayo wanayamaliza kwenye ofisi bila kuyaleta hadharani, yale ambayo Roho Mtakatifu anawapa kibali cha kuyakemea hadharani wanafanya hivyo bila kujalisha wangapi watajisikia vibaya.
Hii ndio faida ya kusoma Neno la Mungu, unakuwa unajua mambo mengi sana ambayo yanakufanya usiwe na maswali mengi yasiyo na majibu sahihi. Nakusihi sana Biblia yako iwe rafiki yako katika kuisoma, utapata maarifa mengi ya kukusaidia katika maisha yako ya wokovu.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com