
Karibia kila mtu unayeweza kuongea naye kuhusu habari za Mungu, wengi huonyesha wanampenda sana Mungu, na wapo wanaonyesha wanamjua sana Mungu kupitia neno lake.
Lakini ukija kwenye maisha yake anayoishi, yanatoa tafsiri nyingine tofauti kabisa na yale maneno yake aliyokuwa anaongea. Mambo anayoyafanya ni machukizo mbele za Mungu, wala hakuna tendo jema ambalo linampendeza Mungu wake.
Yapo mapungufu ambayo yapo kwa kila mwanadamu, madhaifu ambayo wakati mwingine yanamfanya mwanadamu amkosee Mungu wake. Lakini hayo ni tofauti kabisa na yule mtu ambaye anakuwa anafanya mambo mabaya ya waziwazi mbele za Mungu.
Kutamka mdomoni kuwa tunampenda sana Mungu au tunamjua sana Mungu, hakuwezi kutufanya tuonekane tupo vizuri mbele za Mungu. Kumjua Mungu alafu unatenda dhambi za waziwazi bila uoga, huko ni kujidanganya mwenyewe.
Kukiri kwetu kuwa tunamjua sana Mungu wetu, kunapaswa kuendana na vile tunaishi na kuendana katika imani yetu, hivyo ndivyo inavyoweza kututambulisha kuwa sisi tunamjua kweli Mungu au tunaongea tu mdomoni.
Kiwango cha kumjua Mungu kunamfanya mtu aishi vile Neno lake linavyomwelekeza aishi, kwa neema ya Mungu mtu ataweza kuishi maisha yanayompendeza Mungu.
Rejea: Wanakiri ya kwamba wanamjua Mungu, bali kwa matendo yao wanamkana; ni wenye machukizo, waasi, wala kwa kila tendo jema hawafai. TIT. 1:16 SUV.
Usiwe miongoni mwa watu wanaokiri kwa vinywa vyao kuwa wanamjua sana Mungu, alafu ukitazama matendo yao unaona yanapishana na maneno yao walioyokuambia au uliyoyasikia wakisema kwa vinywa vyao.
Kukiri kwetu kuwa tunamjua Mungu hakutoshi, kadri tunavyozidi kumjua kupitia Neno lake tunapaswa kubadilika na kuonyesha kwa matendo kuwa watu hawa wanamjua Mungu wao kweli.
Wale wasiomjua Mungu wao, wanaweza wakawa wanaenenda kama watu walio gizani, hawaoni mbele wala nyuma. Wanaweza kufanya jambo lolote lisilofaa huku wakikiri kwa vinywa vyao kuwa wanamjua Mungu.
Kama umeamua kuokoka, hakikisha uhusiano wako na Mungu unaongea kwa uwazi kupitia matendo yako kuwa huyu mtu kweli anamjua Mungu wake. Barua yako inakuwa inasomwa vizuri na watu wote, na wasiomjua Yesu Kristo wanakuwa wanakiri wenyewe kuwa unaye aliye hai ndani yako.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com