
Misingi ya nchi na mbingu ni kazi ya Bwana, zote zitachakaa na kuharibika kabisa, lakini yeye aliyeziumba mbingu na nchi, hachakai wala habadiliki, wala hazeeki, ni yeye yule jana na leo, na hata milele.
Ikiwa ni hivyo tunapaswa kuwekeza akili zetu zote kwake maana ni zake pia, nguvu zetu zote kwake maana ni zake pia, mioyo yetu yote maana ni ya kwake pia. Maana vitu vyote vinaweza kubadilika na kutoweka kabisa ila yeye ni yeye yule jana na leo na hata milele.
Hachoki wala hazeeki, wala hafi, wala hapotei, siku zote yupo, hata kabla ya kuumbwa kwa misingi ya nchi na mbingu, yeye alikuwepo tangu mwanzo. Na vyote vinavyoonekana na visivyoonekana aliviumba yeye mwenyewe kwa mikono yake.
Katika maeneo ambayo unapaswa kuwekeza muda wako mwingi ni yale mambo ambayo yanakufanya umtukuze Mungu, yale mambo ambayo yanamfanya Yesu wako atukuzwe na jamii, yale mambo ambayo yanakufanya uhusiano wako na Mungu uendelee kuwa imara zaidi.
Vyote vizuri ulivyonavyo vinachoka kabisa na kutoweka ila Mungu wetu yupo pale pale, utazaliwa na kuondoka duniani, lakini yeye ataendelea kudumu milele. Haijalishi utafikiri hakuna Mungu, hilo haliwezi kuzuia chochote isipokuwa siku ya mwisho utaenda kukutana naye, na mahali pale utakapostahili ndio utatupwa humo.
Usije ukafika mahali ambapo utaanza kufikiri Mungu wetu amechoka au amezeeka, Mungu wetu hachoki wala hazeeki kamwe, ni yeye yule jana na leo, na hata milele. Habadiliki kama mwanadamu au kitu chochote kile.
Rejea: Na tena, Wewe, Bwana, hapo mwanzo uliitia misingi ya nchi, Na mbingu ni kazi za mikono yako; Hizo zitaharibika, bali wewe unadumu; Nazo zote zitachakaa kama nguo, Na kama mavazi utazizinga, nazo zitabadilika; Lakini wewe u yeye yule, Na miaka yako haitakoma. EBR. 1:10-12 SUV.
Zipo elimu nyingi zimeinuka siku hizi, kwahiyo ni muhimu sana kukumbushana haya, ni muhimu sana kufundishana haya. Usije ukafika mahali ukaanza kufikiri kinyume na maandiko matakatifu labda kutokana na mazungumzo potovu uliyokutana nayo kwa watu wasiojua Neno la Mungu.
Hayo maandiko yanatuonyesha wazi vyote vitakachakaa kama nguo ila Mungu wetu hachakai, atabaki kuwa yule yule siku zote, hii ni habari njema kabisa kwa wakristo wote duniani.
Tunaye Mungu ambaye yupo miaka yote, vyote vinapita ile yeye yupo vile vile, fasheni zote za dunia hii zitapita ila fasheni yake haipitwi na wakati. Gari lako utalinunua zuri sana ila itafika wakati itapitwa na wakati na kuja muundo mwingine mzuri zaidi.
Nyumba yako utajenga nzuri sana ila itafika wakati itachakaa tu, hata kama utaipiga rangi nzuri bado itaonekana ni ya zamani tu, lakini Mungu wetu yupo vile vile siku zote.
Jivunie hili katika maisha yako ya wokovu, unaye Mungu ambaye hapitwi na wakati, unaye Mungu ambaye hazeeki kamwe, unaye Mungu ambaye hafi, endelea kumtumainia siku zote za maisha yako.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com