
Kuelekezana njia sahihi kila siku ni jambo la msingi sana kwa kila mmoja wetu, bila kufanya hivyo tutajikuta Shetani anamchukua mmoja mmoja na kumtumikisha anavyotaka yeye.
Kueleweshana ni muhimu sana kwa kila mkristo, yapo mambo tunaweza kujikuta tunafanya sana ila katika uhalisia hayo mambo tunayofanya ni kosa mbele za Mungu.
Pale anapotokea mtu anayeelewa unachokifanya ni kosa mbele za Mungu, mtu huyo anapaswa kukuelekeza njia sahihi ya wewe kufuata. Unaweza usielewe sana ila ujumbe utakuwa umekufikia kuwa unachokifanya ni kosa mbele za Mungu.
Kuonyana ni muhimu sana, japo wapo watu hawapendi kuonywa kuhusu yale waliyofanya na yakawa yanakiuka maadili ya mtu aliyeokoka. Lakini anapoonywa wengi huona sio uungwana, na wakati mwingine hujisikia vibaya.
Mtu anayeelewa maandiko vizuri atakuwa ameona amekutana na mtu mzuri wa kumsaidia, kwa maana nyingine nzuri zaidi tunaweza kusema watu wanaoweza kukuambia ukweli pasipo unafiki, na wenye nia kweli ya kukuona umekaa vizuri.
Ujue umekutana na kitu ambacho ni adimu sana katika maisha yako, ndivyo unapaswa kufurahia pale Mungu anapokukutanisha na mtu mwenye ujasiri wa kukuonya kwa nia njema kabisa ya kukufanya ukae vizuri.
Rejea: Lakini mwonyane kila siku, maadamu iitwapo leo; ili mmoja wenu asifanywe mgumu kwa udanganyifu wa dhambi. EBR. 3:13 SUV.
Mtu anayekuonya au anayekuelekeza pale ulikosea, mtu huyo hapaswi kuchukuliwa kikawaida sana, anapaswa kuchukuliwa kwa uzito mkubwa sana katika maisha yako.
Usiogope kuonywa kuhusu yale ambayo utaambiwa, maana ni agizo ambalo tumepewa wana wa Mungu, kama ni agizo ambalo tumepewa hatupaswi kulipuuza na kuliona la kawaida.
Tumeagizwa tuonyane kila siku pale itakapotokea tunapaswa kufanya hivyo, umemwona mwenzako anaenda kinyume na maadili ya mtu aliyeokoka. Usiache kumweleza na kumwelekeza njia sahihi ya yeye kufuata, utakuwa umefanya jambo la maana sana.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com