Uhusiano wako mzuri na Mungu unaweza kukufanya uwe na uwezo wa kufunuliwa mengi sana, ambayo mtu mwingine asiyemjua Mungu hawezi kuwekwa wazi yale yasiyoonekana haraka kwa macho ya nyama.

Bidii ya mtu ya kulijaza Neno la Mungu moyoni mwake, inamfanya aendelee kutiwa nuru zaidi ya kufahamu yale mambo ya rohoni, yale ambayo kwa kawaida usingeweza kuyajua kwa haraka kwa mtu.

Mara nyingi tunaingia kwenye mitengo mibaya na watu wasiofaa, kwa sababu ya kutokuwa na uhusiano mzuri na Mungu wetu au kukosa maarifa ya Neno la Mungu. Laiti kama uhusiano wetu na Mungu ungekuwa vizuri, tungekuwa na uwezo wa kufahamu yale yaliyojificha alafu yana madhara kwetu.

Unaweza ukakutana na mtu anaonekana ni mwema sana, kwa kuwa hujui mengi zaidi kuhusu yeye unaweza kufikiri ni kweli ndivyo alivyo. Lakini ukiwa na uhusiano mzuri na Mungu wako, Neno lake limejaa kwa wingi moyoni mwako, ni rahisi kufunuliwa mengi juu ya huyo mtu.

Ukishafunuliwa unaweza kuona ule mwonekano wake wa nje, ni tofauti kabisa na tabia yake ilivyo, kwanini ni tofauti, kwa sababu yapo mambo mabaya anayoyafanya bila wewe kujua. Na yapo mambo mazuri sana anafanya bila wewe kujua japo kwa mwonekano wake wa nje anaonekana wa kawaida.

Rejea: Wala hakuna kiumbe kisichokuwa wazi mbele zake, lakini vitu vyote vi utupu na kufunuliwa machoni pake yeye aliye na mambo yetu. EBR. 4:13 SUV.

Ikiwa Yesu Kristo yupo ndani yako na Neno lake lipo kwa wingi ndani yako, vitu vingi sana vitakuwa wazi kwako, wakati rafiki yako anafikiri anakuficha kitu na kukifanya kwa siri. Ndani yako unaweza kupewa picha yake na ukaona vile maisha yake halisi yalivyo.

Wakati watu wanatafuta kujua kama mume/mke aliyenaye ni mwaminifu katika ndoa yake ama la, kwa mwana wa Mungu aliye na Neno la Mungu la kutosha moyoni mwake. Hilo sio jambo gumu kwake, atambua upesi sana.

Pia wale walio na wachumba au marafiki wanaoelekea kwenye uchumba hadi ndoa, mara nyingi huwa wanakuwa na mashaka kama wana watu ambao ni waaminifu. Lakini aliyeokoka sawasawa na ana Neno la Mungu la kutosha kwake sio shida kuhusu hili.

Sio kwamba anasema kitu ambacho hakipo, Neno la Mungu linaweza kutambua makusudi ya moyo wa mtu, au tabia ya mtu ilivyo kwa njia ambayo ni rahisi kabisa kwa mwana wa Mungu aliye hai.

Rejea: Maana Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo. EBR. 4:12 SUV.

Andiko hilo linaweza kuonekana ni jepesi sana kwako kama utalisoma kikawaida, au kama utalisoma haraka haraka, lakini ukilisoma kwa makini na katika roho utaona ni andiko lililobeba vingi sana na vyenye umhimu mkubwa katika maisha ya mkristo.

Hakikisha unasoma Neno la Mungu kila siku, kupitia usomaji wako utaona maeneo mengi sana katika maisha yako ya wokovu yakibadilika na kukua zaidi hatua kwa hatua. Na utaacha kutabishwa baadhi ya maeneo katika maisha yako ya kiroho na kimwili.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com