
Eneo ambalo huwa halionekani haraka kama lina matunda mazuri sana, ni hili la kujitoa katika kazi ya Mungu, na kuonyesha upendo kwa wengine, kwa kuwahudumia watumishi wa Mungu wanapokuwa kwenye huduma.
Kwa macho ya nyama ni kazi ambayo haina faida yeyote, na inaonekana kwa wengine ni kupoteza muda tu, lakini mtu ambaye ameokoka sawasawa na Neno la Mungu lipo ndani yake. Hili haliwezi kuwa jambo gumu kwake, wala haliwezi kuwa na maswali mengi.
Kujitoa kwa ajili ya kazi ya Bwana, au kujitoa kwa kazi yeyote ile halali, uwe na uhakika Mungu hataisahau kazi yako, ile bidii yako uliyokuwa unaionyesha katika kazi uliyokuwa unaifanya. Bidii hiyo ya kazi itakufanya upokee matunda mazuri kwa kile ulifanya.
Haitajalisha kwa sasa watu wanaona kawaida au wanachukulia kwa namna ya kujitoa sana bila kujipumzisha, usiposikiliza maneno ya watu na ukaendelea kutenda kazi yako kwa uaminifu. Uwe na uhakika Mungu hataisahau kazi yako.
Rejea: Maana Mungu si dhalimu hata aisahau kazi yenu, na pendo lile mlilolidhihirisha kwa jina lake, kwa kuwa mmewahudumia watakatifu, na hata hivi sasa mngali mkiwahudumia. EBR. 6:10 SUV.
Kuna mambo wanadamu wanaweza kusahau kabisa kama uliwahi kuwafanyia ila fahamu kwamba Mungu hataisahau kazi yako, Mungu hatausahau upendo wako ulionyesha kwa watumishi wa Mungu na wale waliokosa tumaini la maisha.
Kazi yako njema inajulikana mbele za Mungu, ikiwa inajulikana mbele za Mungu haina haja kuwa na shaka pale watu wanapoonyesha kutokujali au kutotoa ushirikiano wao. Ipo siku Mungu atawaonyesha kwa uwazi kabisa kuwa ulikuwa unafanya kazi njema.
Endelea kutenda mema, endelea kutenda kazi ya Bwana vizuri, na endelea kuonyesha upendo kwa wengine. Mungu hataisahau hata kazi moja, zote zinajulikana mbele za Mungu na zina hesabu zake siku ya mwisho.
Unapoamka, unapolala, unapotembea, au unapokuwa umekaa, uwe unafahamu kazi yako haitasahaulika mbele za Mungu, kazi yako alama, upendo wako kwa wengine ni alama yako mbele za Mungu.
Mungu akusaidie sana utende kazi njema, na uonyeshe upendo wako ulionao kwa wengine, hii itakufanya uonekane mbele za Mungu. Mungu mwenyewe ndiye atakayekutambulisha kwa wale ambao walikuwa wanakuchukulia kawaida, kuwa wewe ulikuwa unafanya kazi njema.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com