
Ukiwa mtu mzima au ukiwa mzazi, yapo mambo mengi watoto wako wanajifunza mambo mbalimbali kupitia wewe. Ukiwa na mambo yasiyofaa ujue watoto wako wanachukua na kuanza kuishi vile ambavyo walikuwa wanamwona mzazi wao anafanya.
Ikiwa matendo ya mzazi ni mazuri sana ya kumpendeza Mungu, pamoja na kuwa mzazi anapaswa kumkuza mtoto wake katika maadili mazuri ya kumjua Mungu na kumpendeza Mungu. Bado mzazi ana mchango mkubwa kwa mtoto wake kupitia matendo yake.
Jambo lolote linalochukiza likifanywa na mtu mzima, ni rahisi kumchukiza sana mtoto au likamuumiza sana mtoto, kutokana na aliyefanya ni mtu mkubwa. Na sio mtoto ndiye aliyefanya hicho kitu bali ni mtu mzima anayepaswa wengine wajifunze kupitia yeye.
Pia ni rahisi sana kama mtu mzima atafanya jambo la kuwabariki watu, moja kwa moja yule mdogo atabarikiwa na yule mkubwa, maana ni mtu anayetazama wengine waliomzidi kiumri au kihuduma au kiuchumi kwa kile wanachofanya.
Kile kizuri wanachofanya kinakuwa kinazaa matunda ya kuwabariki wale wadogo wanaowatazama wakubwa zao wanavyofanya vizuri kwenye maeneo yao. Hicho kinawafanya watu wajue umhimu wa kuwa kiwango fulani kwa ajili ya utukufu wa Mungu.
Siku zote mdogo hubarikiwa na mkubwa, vile vile mdogo anaweza kuchukizwa na mkubwa, vyote vinawezekana kuwepo ila wewe unapaswa kukaa kwenye eneo zuri la kuwa baraka kwa wengine.
Rejea: Wala haikanushiki kabisa kwamba mdogo hubarikiwa na mkubwa. EBR. 7:7 SUV.
Vizuri sana kuwa sehemu ya kuwabariki wale walio wadogo, uwe mkubwa kwenye ofisi yako, uwe mkubwa kwenye jamii yako, uwe mkubwa wa umri. Unapaswa kuwa sehemu ya kuwabariki wale wale, wale wanaokutazama kama kiongozi wao, au kama mzazi wao au kama ndugu yao.
Ukubwa unaweza ukawa wa cheo au unaweza ukawa wa umri, unapaswa kuwa mtu wa baraka kwa unaowagoza au wanaokutazama kama mfano wao. Hili ni la muhimu sana kuzingatia ili ufanye vizuri kwenye eneo hili.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com