Shida ambayo inawatesa watu wengi waliomwamini Yesu Kristo, na kuwa ndani ya wokovu kwa muda fulani, wengi huwa hawakubali kuonywa kuhusu yale wanayoyatenda yasiyompendeza Mungu.

Mtu mwingine akionywa au ukimrekebisha kuhusu mwenendo wake mbaya, anaona kama vile umemfanyia jambo lisilo sahihi kwake. Ama mwingine anaweza kuona hustahili kumweleza ukweli kutokana na anavyokuona ulivyo.

Tukiwa kama watoto wa Mungu tunapaswa kukubali kuonywa au kurekebishwa au kurudiwa, haijalishi anayekurudi yupoje au anaonekanaje. Unapaswa kukubali kurekebishwa au kuelekezwa pale inapobidi uelekezwe.

Mungu anaweza kumtumia mtu yeyote kwako, akakuletea ujumbe wa kukusaidia kutoka katika eneo la kumkosea Mungu wako na kuwa kwenye eneo la kumpendeza Mungu wako.

Mtoto wa Mungu anapaswa kukubali kurekebishwa, au kuonywa, au kurudiwa, bila kufanya hivyo kila mmoja atajiendea anavyojua yeye mwenyewe. Na hakuna atakayeweza kumsaidia mwenzake, maana kila mmoja atakuwa anajiona yupo sahihi.

Rejea: Basi kama mkiwa hamna kurudiwa, ambako ni fungu la wote, ndipo mmekuwa wana wa haramu ninyi, wala si wana wa halali. EBR. 12:8 SUV.

Ikiwa mtoto wako unaweza kumrekebisha pale anapokosea, ama ikiwa hutamani mtoto wako awe na tabia fulani isiyo nzuri. Unahakikisha unamwelekeza na kumchapa fimbo pale anapoonekana kukosa nidhamu, ujue ndivyo ilivyo na kwa Mungu wetu kwetu.

Anaweza asikujie mtumishi moja kwa moja ila kupitia usomaji wa Neno la Mungu, ukakutana na maonyo yanayokutaka urekebishe njia zako zisizokuwa nzuri. Kama utatii hiyo sauti iliyokuambia ujirekebishe, uwe na uhakika maisha yako yatakuwa na amani.

Kurudiwa kwa mwana wa Mungu ni jambo ambalo anapaswa kuliona ni la maana sana kwake, maana kupitia kumrudi mtu kumefanyika baraka kwa wengi waliotii kuonywa na kuelekezwa mahali pa kupita.

Usifikiri mtoto tu ndio anastahili kurudiwa pale anapokosea, hata wewe ambaye umetoka kwenye utoto kimwili, unastahili kurekebishwa pale unapokosa au unapopaswa kupitia njia sahihi unahitaji upate mtu atakayekuelekeza vizuri.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com