Unajua kuna watu wanasema wameokoka lakini bado mambo ya dunia yamewateka fahamu zao, hawaoni vibaya kumtenda Mungu dhambi huku wanaingia kwenye nyumba za ibada.

Wengine sio kuingia tu kwenye nyumba za ibada, wapo wanafanya na huduma madhabahuni lakini kuna vitu vibaya wanavifanya kama wale ambao bado hawajampokea Kristo kama Bwana na mwokozi wao.

Wengine wanaingia kwenye nyumba za ibada ila tegemeo lao kubwa ni kwa miungu mingine, pamoja na kuonyesha ushirika wao na wengine kanisani. Mambo mengi wanategemea msaada kwa miungu mingine, na huku wapo kanisani.

Watu kama hawa bado hawajajua wa kumtumikia ni yupi au wa kumwabudu ni yupi, maana wangejua Mungu wanayemwabudu wasingekimbilia kutafuta msaada kwa waganga wa kienyeji. Wangejua Mungu waliyenaye ni mkuu sana kuliko miungu mingine yeyote ile.

Kwa kutojua hilo mtu anakuwa yupo njia mbili, anategemea kupata msaada kwa Yesu, na wakati mwingine anaenda kutafuta msaada kwa miungu mingine. Bila kujua hicho anachokifanya ni chukizo kubwa sana mbele za Mungu.

Ukiwa kama mkristo au mtu uliyeamua kumpokea Yesu Kristo kama Bwana na mwokozi wako, na ukakiri kwa kinywa chako, unapaswa kuchagua kumfuata au kutumikia mmoja tu na sio kuongezea na mambo mengine yaliyo machukizo mbele za Mungu.

Rejea: Nanyi kama mkiona ni vibaya kumtumikia BWANA, chagueni hivi leo mtakayemtumikia; kwamba ni miungu ile ambayo baba zenu waliitumikia ng’ambo ya Mto, au kwamba ni miungu ya wale Waamori ambao mnakaa katika nchi yao; lakini mimi na nyumba yangu tutamtumikia BWANA. YOS. 24:15 SUV.

Ndugu yangu umechagua kumtumikia Mungu au miungu mingine? Umechagua kujiweka kwa Yesu mzima mzima au bado mambo ya dunia yanakuvutia uyafanye? Neno la leo linatuambia tuchague moja, kumtumikia BWANA au miungu ya baba zetu.

Vyote vipo ndani ya uwezo wako, unaweza kuamua kujiweka kwa Yesu Kristo kwa asilimia zote, na bado unao uamzi wa kuchagua kuitumikia miungu mingine. Najua unayesoma ujumbe huu unampenda Yesu, kama unampenda Yesu usikubali kuwa mtu wa kujichanganya na mambo mabaya.

Umeamua kuokoka maanisha kweli katika hilo, wala asiwepo mtu yeyote wa kukuyumbisha juu ya hili, maana unaweza ukawa umeokoka alafu bado tabia yako inaonyesha bado hujaokoka. Itaonyesha hivyo kama bado hujachagua kwa kumaanisha kufuata njia sahihi ya Yesu Kristo.

Chagua leo na nyumba yako umtumikie BWANA, bila kujalisha kelele za nje zinazopigwa juu yako, ukifanya hivyo utampendeza Mungu na maisha yako ya wokovu yatakuwa salama siku zote za maisha yako.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com