
Hekima ya duniani inaweza isiwe na viwango vya kuweza kuhimili baadhi ya mambo, na wakati mwingine inaweza isiwe na nguvu sana kama ilivyo hekima ya kiMungu.
Mtu anaweza akawa mjuzi sana wa mambo, akawa na uwezo wa kung’amua baadhi ya mambo, watu wakawa wanamtegemea kwa hekima yake aliyonayo. Hekima yenyewe inaweza isiwe ya mtu aliyeokoka ila anayo hekima ya duniani.
Mtu huyu hadi kuwa na hekima ya duniani, anaweza akawa anajifunza sana kupitia vitabu mbalimbali za watu walioviandika, kupitia usomaji wao wakawa na ufahamu mkubwa wa kuweza kuwasaidia wengine.
Pamoja na kuwa na hekima ya duniani, na inatumika kuamua mambo mengi na mengine ni mambo nyeti ambayo yanahitaji watu makini, na wenye uwezo mkubwa wa kuweza kufikiri zaidi.
Lakini pamoja na kuwa na uwezo mkubwa wa kufikiri, na pamoja na kuwa na hekima nyingi sana, bado wamepungukiwa na hekima ya kiMungu, hekima itokayo juu mbinguni.
Hekima ambayo amwaminiye hupewa kama zawadi, hekima ambayo huipata mtu aliyeokoka kupitia usomaji wake wa maarifa ya Neno la Mungu. Hii akiwa nayo mtumishi wa Mungu ni bora sana kuliko hekima zote unazozijua wewe.
Rejea: Lakini hekima itokayo juu, kwanza ni safi, tena ni ya amani, ya upole, tayari kusikiliza maneno ya watu, imejaa rehema na matunda mema, haina fitina, haina unafiki. YAK. 3:17 SUV.
Ndugu yangu sijui umechagua fungu lipi ila fahamu kwamba kuwa na hekima ya kiMungu ni nzuri sana, cha msingi ni wewe kuweka bidii katika kusoma Neno la Mungu. Taratibu utaanza kuona kuna mabadiliko ndani yako yanajengeka.
Tamani sana hekima kutoka mbinguni, usiishi tu ilimradi unaishi, au unaweza ukawa unafikiri nitaipataje hiyo hekima, ni kuendelea kuweka bidii katika kusoma Neno la Mungu.
Huku ukiendelea kumwomba Mungu atende jambo juu ya maisha yako, Ukiwa unajua upo umhimu wa kuendelea kujifunza zaidi. Vile unavyozidi kujifunza zaidi ndivyo unavyozidi kuongezeka kiwango chako chako.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com